1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yamfutia hatia Chui

18 Desemba 2012

Mbabe wa kivita Ngudjolo Chui, alikuwa akituhumiwa kuhusika na mauaji, ukatili na ubakaji katika eneo la Ituri mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, muongo mmoja uliopita.

https://p.dw.com/p/174gJ
Mbabe wa kivita Mathieu Ngudjolo Chui
Mbabe wa kivita Mathieu Ngudjolo ChuiPicha: AFP/Getty Images

Majaji wa Mahakama ya Kimataifa inayoshughulikia kesi za uhalifu wa kivita, ICC, yenye makao yake mjini The Hague nchini Uholanzi, imemuondolea mashtaka ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu mbabe wa kivita wa Kongo, Ngudjolo Chui.

Uamuzi huo ni wa pili katika historia ya mahakama hiyo ya uhalifu na ni uamuzi wa kwanza wa kufutiwa mashtaka mtuhumiwa, hatua ambayo inaonekana kama ni pigo kwa waendesha mashtaka wa ICC ambao  kwa mujibu wa majaji wameshindwa kutoa ushahidi wa kumuhusisha Ngudjolo moja kwa moja na mauaji ya Kaskazini Mashariki ya Kongo yaliyotokea mwaka 2003. Aidha uamuzi uliotolewa leo Jumanne (18.12.2012) pia unazusha mashaka kuhusu kesi dhidi ya mtuhumiwa mwengine wa mauaji hayo mbabe wa kivita, Germain Katanga, anayeshtakiwa kwa makosa kama yaliyokuwa yakimkabili Chui.

Mwendesha Mashtaka wa ICC Fatou Bensouda,
Mwendesha mashtaka wa ICC Fatou BensoudaPicha: DW

Ushahidi mzito wakosekana

Mwezi uliopita majaji waliahirisha kesi ya Katanga katika hatua ambayo baadhi ya wasomi wanasema huenda ikarahisisha kumtia hatiani. Mapigano ya Kaskazini mashariki mwa mkoa wa Ituri  yalikuwa ni mapigano ya kikabila yaliyochochewa na suala la ardhi na mali, mojawapo ya chanzo cha mizozo iliyozuka katika nchi nzima ya Kongo katika mwaka 1998 hadi 2003 na iliyozihusisha nchi jirani. Halikadhalika mapigano ya Ituri yanamuhusisha pia Bosco Ntaganda ambaye anatakiwa na mahakama hiyo ya ICC kwa kutuhumiwa kuhusika na uhalifu wa kivita katika mzozo huo.

Waendesha mashtaka wanasema Ngudjolo Chui alitoa amri kwa wapiganaji kuzifunga barabara za kuingia na kutoka kijiji cha Bogoro mnamo mwezi wa Februari mwaka 2003 kwa lengo la kufanyika mauaji ya raia waliokuwa wakijaribu kukimbia. Inadaiwa wanawake na watoto walichomwa wakiwa hai ndani ya nyumba zao na kusababisha vifo vya watu 200 wakati na baada ya mashambulizi dhidi ya kijiji hicho wakati wapiganaji wa kabila la Walendu na Ngiti walipodaiwa kuziteketeza nyumba za wakaazi wa kijiji hicho ambao wengi walikuwa ni kutoka kabila la Wahema.

Rufaa itafanikiwa?

Wakili wa mahakama, Nick Kaufmann, amesema tukio hilo lilikuwa fupi na la kusikitisha lakini upande wa waendesha mashtaka umeshindwa kuchunguza ipasavyo mamlaka ya uongozi na utoaji amri kuhusiana na shambulizi hilo la kijiji cha Bogoro. Mashahidi waliosimama dhidi ya Ngudjolo hawakutoa ushihidi wa kutosha kuwashawishi majaji. Fatou Bensouda ambaye ni mwendesha mashataka mkuu mpya wa ICC tangu mwanzoni mwa mwaka huu, hata hivyo amewaomba majaji kumuweka kizuizini Ngudjolo hadi pale itakapokatwa rufaa.

Jean Bosco Ntaganda kiongozi wa M23 ahusishwae na vita vya Ituri
Jean Bosco Ntaganda kiongozi wa M23 ahusishwae na vita vya IturiPicha: dapd

Pamoja na hilo lakini wataalamu wa kisheria wanasema itakuwa vigumu kuubatilisha uamuzi wa mahakama kwa sababu hakuna ushahidi mpya utakaoweza kutolewa wakati wa kusikilizwa rufaa. Watetezi wa haki za binadamu kama vile Shirika la Human Rights Watch kwa hivyo wanahisi uamuzi wa majaji wa ICC wa kumuondolea mashtaka Ngudjolo unawaacha wahanga wa Bugoro na wa maeneo mengine ambako vikosi vyake vilifanya mauaji, kutotendewa haki.

Makaburi ya pamoja Ituri
Makaburi ya pamoja IturiPicha: AP

Mkurugenzi wa shirika hilo anayehusika na masuala ya sheria za Kimataifa, Geraldine Mattioli-Zeltner, ametoa mwito kwa waendesha mashataka wa ICC kuimarisha uchunguzi wake kuhusiana na wahusika wa mauaji ya Ituri ikiwa ni pamoja na maafisa wa ngazi za juu wa Kongo, Rwanda na Uganda.

Mwandishi:Saumu Yusuf

Mhariri:Josephat Charo