1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IMF yaonya tatizo la kiuchumi laenea kwa nchi maskini

Mohammed, Munira/REUTERS4 Machi 2009

Nchi za Afrika zaathirika

https://p.dw.com/p/H5W7
Mkurugenzi mkuu wa fuko la fedha la kimataifa Dominique Strauss-KahnPicha: AP

Hazina ya fedha ulimwenguni, IMF imeonya kuwa mzozo wa kimataifa wa kiuchumi utaathiri mataifa 22 yasiojiweza na takriban dola bilioni 25 za ufadhili zinahitajika na mataifa hayo kuzuia yasiporomoke kabisa kiuchumi. Kulingana na IMF, wanakisia iwapo hali hii ya kiuchumi itaendelea basi mataifa haya 22 yatahitaji msaada zaidi wa kifedha unaokisiwa kuwa dola bilioni 140 ili uchumi wake usiangamie." Mataifa yanayoendelea huenda yakakumbwa na matatizo makubwa."

Ndio matamshi ya mkurugenzi mkuu wa shirika la IMF Dominique Strauss Kahn, akitaja hali hii kama msukusuko wa tatu wa mzozo huu wa kiuchumi ambao umesambaa kutoka masoko ya fedha na ya mikopo hadi uchumi wa utumiaji wa bidhaa.

Jinsi hali ilivyo, Dominique anasema anatarajia mataifa mengi yatatafuta mkopo zaidi kutoka IMF ilhali walio na mikopo tayari wanatazamiwa kuongeza viwango vya kukopa.

Shirika la IMF limezindua ripoti mpya, inayoangazia athari za mzozo huu wa kiuchumi katika mataifa yenye mapato ya chini.

Makisio ya shirika la IMF, yanaonyesha kwa ujumla uwiano wa malipo katika mataifa 38 huenda ukafikia dola bilioni 165, kiasi hiki pia kinatarajiwa kuongezeka hadi dola bilioni 216 iwapo mzozo huu wa kiuchumi hautapata nafuu.

Athari zaidi kulingana na shirika la IMF ni kwamba fedha za akiba za mataifa haya pia zinatazamiwa kupungua, ukilinganisha na bidhaa za kutoka nje kwa muda wa miezi mitatu na matokeo ni hasara kubwa, dola bilioni 25 au aslia mia 80 ya msaada unaotolewa kwa mataifa masikini katika miaka mitano.

Nchi zinazoendelea zimepunguza mahitaji yake ya bidhaa zinazotoka nje ilhali ruzuku zinazotolewa na wafanyikazi wake waliohamia katika mataifa ya nje kwa familia zao pia zimepungua sana kutokana na kudorora kwa uchumi Marekani na mataifa ya Ulaya. Ufadhili wa kigeni katika mataifa yenye mapato ya chini pia unatarajiwa kupungua.

Hata hivyo afueni kwa mataifa haya maskini ni kupungua kwa bei za bidhaa muhimu kama vile mafuta na vyakula- hivyo hamna tishio la mfumko wa bei.

Shirika la IMF pia limeyaorodhesha mataifa 26 kuwa yenye uwezekano mkubwa wa kukabiliwa na mzozo huu wa kiuchumi, lakini ikaongeza uwezekano sio mkubwa kuwa mataifa haya

yataathirika hivyo hakuna dharura ya ufadhili zaidi. Nchi tisa za Kiafrika, kama vile Zambia, Angola, Liberia, Sudan, Burundi, Nigeria ni miongoni mwa mataifa hayo. Mengine ni Albania Mongolia, Moldova na Vietnam.

Kwa ujumla uwiano wa hazina za mataifa yanayoendelea unatazamiwa kudorora kwa aslia mia 2.5 ya pato jumla la kitaifa mwaka 2009.

Mbali na changamoto hizi za mporomoko wa kiuchumi, shirika la IMF limeyasisitizia mataifa ya kifadhili yasisitishe msaada wao wa kifedha kwa mataifa masikini na pia kutimiza ahadi zao za kuongeza maradufu misaada ya kifedha kwa Afrika itiamiapo mwaka wa 2010.