India na Ufaransa kupanua uhusiano
25 Januari 2008Matangazo
India na Ufaransa zimesema leo kwamba zitapanua uhusiano wao mbali na uuzaji wa silaha. Ufaransa itaanzisha ushirikiano katika maswala ya nishati ya nyuklia mara tu India itakapofaulu kuingia katika soko la nishati ya nyuklia la kimataifa. Waziri mkuu wa India, Manmohan Singh, amesema leo kwamba amekubaliana na rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa anayezuru India, juu ya kuuendeleza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Rais Sarkozy amesema mazungumzo yamekamilika kuhusu mkataba wa ujenzi wa vinu vya nyuklia, sehemu muhimu ya teknolojia ya Ufaransa ambayo inaonekana kuwa muhimu kwa juhudi za India kutosheleza mahitaji ya nishati ya uchumi wake unaokua kwa kasi ya asilimia tisa.
Hapo kesho rais Sarkozy, atakuwa mgeni wa heshima katika sherehe za kuadhimisha sikukuu ya jamhuri. Maafisa wa usalama nchini India wameanza juhudi za kuimarisha usalama huku maadhimisho ya sikukuu ya jamhuri yakitarajiwa kufanyika hapo kesho.