India na Pakistan zajaribu kukaribiana
25 Februari 2010Waziri wa Mambo ya Nje wa India Nirupama Rao na waziri mwenzake wa Pakistan Salman Bashir hii leo wamekutana mjini New Delhi kwa majadiliano rasmi ya kwanza yaliyokuwa na azma ya kuondoa hali ya kutoaminiana na kupunguza mvutano katika uhusiano wao. Mashambulio ya Mumbai yaliyofanywa na wanamgambo wa kundi la Lashkar-e-Taiba yenye makao yake nchini Pakistan yamesababisha mvutano mkubwa katika uhusiano wa majirani hao wawili wanaodhibiti silaha za nyuklia.
India imeeleza waziwazi kuwa ugaidi ndio mada kuu pekee na inaitaka Pakistan ichukue hatua ya kuuvunja mtandao wa kigaidi kabla ya masuala mengine kuweza kujadiliwa katika utaratibu wa amani ulioanza miaka minne iliyopita. India inasisitiza kuwa Pakistan lazima itatue njama ya mashambulio ya Mumbai yaliyoua watu 166 na waliohusika wafikishwe mahakamani. Vile vile wanamgambo wanaoilenga India wasiruhusiwe kupanga mashambulio yao katika ardhi ya Pakistan.
Lakini Pakistan inashikilia kuwa majadiliano ya hivi sasa yashughulikie pia masuala mengine kama vile mzozo wa Kashmir na jinsi ya kugawana maji. Hapo kabla, Waziri Bashir alipozungumza na waandishi wa habari alisema, yeye amekwenda India kwa matumaini ya kuondosha tofauti zilizokuwepo kati ya majirani wawili. "Sisi tunataka kujadili masuala yote pamoja na India - hata ugaidi, lakini kipaumbele ni Kashmir," aliongezea Waziri wa Nje wa Pakistan. Lakini mbali na Kashmir, Pakistan inatazamiwa pia kugusia madai kuwa India inashiriki katika uasi wa wilaya ya Balochistan nchini Pakistan.
Mazungumzo ya leo yamefanywa huku nchini India ikihofiwa pia kuwa shambulio la bomu lililofanywa katika mkahawa mmoja mapema mwezi huu mjini Pune magharibi ya India, ni mwanzo wa mashambulio yatakayofuata. Watu 16 waliuawa katika shambulio hilo. Ikiwa kweli kutatokea mashambulio mengine nchini India, basi kisiasa itakauwa vigumu sana kwa serikali ya India kufuatiliza maendeleo yo yote yatakayopatikana katika majadiliano ya leo hii. Vile vile haikuwa rahisi kwa India kurejea katika majadiliano hayo na Pakistan kwani umma nchini India unapinga vikali. Lakini India ikishinikizwa na Marekani na ikipungukiwa na suluhu zingine za kidplomasia, haikuwa na budi isipokuwa kuinyoshea mkono Pakistan. Uhusiano mzuri kati ya India na Pakistan ni muhimu pia kwa Marekani kwani hivyo, Islamabad haitokuwa na wasiwasi kwenye mpaka wake na India mashariki mwa nchi na majeshi yake yataweza kupambana na wanamgambo wa Taliban upande wa magharibi unaopakana na Afghanistan.
Mwandishi:Martin,Prema/RTRE
Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed