1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

India yaimwagia Afrika mabilioni ya dola

24 Mei 2011

Katika kile kinachoonekana kama uwekezaji mpya wenye nia ya kuvuna ushawishi katika bara la Afrika, India itatoa dola bilioni 5 kwa mataifa ya bara hilo.

https://p.dw.com/p/11Mn6
Wasichana wa kabila la Maasai nchini Kenya
Wasichana wa kabila la Maasai nchini KenyaPicha: DW

Waziri Mkuu wa India, Manmohan Singh, amesema hii leo (24 Mei 2011) wakati wa mkutano na viongozi wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia, kuwa, India itatoa fedha hizo katika kipindi cha miaka mitatu ijayo kwa msingi wa mikopo ili kuyasaidia mataifa ya Afrika kutimiza miradi yake ya maendeleo.

Singh alianza ziara yake ya siku sita barani Afrika hapo jana, akiahidi msaada wa maendeleo kwa kuwa na mikataba ya kibiashara kwa lengo pia la kuimarisha ukuaji wa uchumi wa India.

Waziri Mkuu huyo wa India anatarajiwa kuizuru Tanzania siku ya Alhamis ambapo atatia saini mikataba kadhaa ya ushirikiano kati ya nchi yake na Serikali ya Tanzania.

Waziri wa serikali ya Sudan ajiuzulu

Sehemu ya viunga vya mji wa Abyei baada ya mapambano
Sehemu ya viunga vya mji wa Abyei baada ya mapambanoPicha: picture-alliance/dpa

Waziri wa Shughuli za Baraza la Mawaziri nchini Sudan, Luka Biong Deng, amejiuzulu wadhifa wake hivi leo, kulalamika kile alichokitaja kuwa ni uhalifu wa kivita katika jimbo la Abyei, linalodhibitiwa na vikosi vya majeshi ya Kaskazini.

Deng, ambaye ni afisa wa ngazi ya juu katika serikali ya Umoja wa Kitaifa, amesema walitarajia kuunda mataifa mawili yatakayokuwa na uhusiano mwema, lakini wenzao wa Kaskazini wanaonekana hawataki amani.

Mwanachama huyo wa chama cha Sudanese People's Liberation Movement (SPLM) na ambaye anatokea jimbo la Abyei linalokabiliwa na mzozo, amesema kuwa hawezi kuendelea kuhudumu katika serikali kuu ya Sudan, kwa sababu vikosi vyake ndivyo vinavyofanya uhalifu huo wa kivita katika jimbo analotokea la Abyei.

Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umesema kiasi ya watu 15,000 wamekimbia ghasia katika eneo hilo, huku hali ikizidi kuwa ngumu. Serikali ya Kaskazini mjini Khartoum imesema wanajeshi wake wako katika eneo hilo kurejesha utulivu, baada ya mashambulizi mabaya yaliyofanywa na vikosi vya Kusini, Alhamis iliyopita.

Mzimbabwe kufikishwa mahakamani kwa maandamano ya Misri

Waziri Mkuu wa Zimbabwe, Morgan Tsvangirai (katikati) akizungumza na mawaziri wenzake
Waziri Mkuu wa Zimbabwe, Morgan Tsvangirai (katikati) akizungumza na mawaziri wenzakePicha: AP

Raia mmoja wa Zimbabwe atafikishwa mahakamani mwezi ujao kwa kuweka maandamano yaliofanyika Misri kwenye mtandao wake wa Facebook.

Gazeti la binafsi Newday limesema mahakama mjini Bulawayo imepanga Juni 10 kuwa tarehe ya kusikilizwa kesi dhidi ya Vikas Mavhuzi anayekabiliwa na makosa ya kutuma risala katika mtandao wa Facebook inayomhusu Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai.

Risala hiyo inadaiwa kusema: "Kilichotokea Misri kimezusha dharuba kali dhidi ya madikteta duniani kote na kwamba hakuna silaha nzito kuliko umoja."

Itakumbukwa kwamba mnamo mwezi Februari, Wazimbabwe 46 walishtakiwa kwa uhaini, walipokamatwa na polisi wakati wakiwa katika mjadala wa hadhara kuhusu matukio nchini Misri.

Wanaharakati 38 waliachiliwa huru baadaye kwa ukosefu wa ushahidi, lakini wengine 6 akiwemo mbunge wa zamani kutoka chama cha Tsvangirai cha MDC, Munyaradzi Gwisai, wakaachiwa kwa dhamana.

NATO yaitwanga tena Tripoli

Miripuko kutokana na mashambulizi ya NATO mjini Tripoli
Miripuko kutokana na mashambulizi ya NATO mjini TripoliPicha: dapd

Serikali ya Libya imesema kiasi ya watu watatu wameuawa na wengine 150 kujeruhiwa wakati ndege za kivita za Jumuiya ya Kujihami ya NATO zilipoushambulia kwa mabomu mji mkuu Tripoli mapema leo.

Zaidi ya mashambulizi ya angani 20 kutoka ndege za NATO yaliutikisa mji mzima katika kile ripoti zinachosema ni mashambulizi makubwa kabisa tangu operesheni hiyo ya angani ilipoanza miezi miwili iliyopita.

Hapo jana, Ufaransa ilitangaza kuwa waoa na Uingereza wanazituma helikopta za kivita kuwashambulia wanajeshi wa Gaddafi kwa kutumia mbinu ya mashambulizi ya awamu.

Ufaransa na Uingereza zimekuwa mara kwa mara zikiunga mkono kuimarishwa kwa operesheni hiyo inayoongozwa na NATO dhidi ya Gaddafi.

Gambia yawahukumu wanajeshi kwa uhaini

Rais Yahya Jammeh (kulia) akiwa na Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad
Rais Yahya Jammeh (kulia) akiwa na Rais wa Iran, Mahmoud AhmadinejadPicha: AP

Mahakama maalum nchini Gambia imewahukumu wakuu wa zamani wa jeshi la ulinzi na la majini vifungo vya hadi miaka 20 jela kwa uhaini, kwa kuhusika na jaribio la mapinduzi mwezi Machi 2006.

Mkuu wa zamani wa majeshi, Lang Tombong Tamba, ambaye tayari alihukumiwa kifo kwa kuhusika katika jaribio la mapinduzi lililoshindwa 2009, alihukumiwa kifungo gerezani pamoja na Sarjo Fofana aliyekuwa mkuu wa jeshi la majini.

Tamba alihukumiwa kifo pamoja na maafisa kadhaa wengine wa ngazi ya juu Julai 2010. Mwezi Machi 2006, serikali ya Gambia ilitangaza imelikandamiza jaribio la mapinduzi la kutaka kumuangusha Rais Yahya Jammeh, ambaye binafsi alitwaa madaraka kwa njia ya mapinduzi 1994.

Tamba, aliyekua wakati huo naibu mkuu wa majeshi, akapandishwa cheo kuwa mnadhimu mkuu. Jammeh anasemekana anaitawala Gambia kimabavu, akiwakandamiza wakosoaji wake na kupuuza wito wa kumtaka aheshimu haki za binaadamu.

Kiongozi huyo ambaye kesho atatimia umri wa miaka 46, anatarajiwa kuwani muhula wa nne wa uongozi katika uchaguzi ujao mnamo mwezi Novemba.

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman