1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaYemen

Israel yashambulia miundombinu ya Wahouthi Yemen

19 Desemba 2024

Israel imeshambulia ngome za waasi wa Kihouthi nchini Yemen mapema Alhamisi na kuua watu tisa. Awali israel ilidungua kombora lililofyatuliwa kutoka Yemen.

https://p.dw.com/p/4oLw9
Israel | Ndege za kivita za Israel
Ndege za kivita 14 za Israel zimehusishwa katika mashambulizi dhidi ya miundo mbinu ya nishati na bandari nchini Yemen Disemba 19, 2024. (Picha ya maktaba)Picha: Ilia Yefimovich/dpa/picture alliance

Kulingana na vyombo vya habari vya Israel, mabaki ya kombora lililodunguliwa yalianguka karibu na mji mkuu Tel Aviv na kuharibu vibaya shule moja. Hata hivyo msemaji wa jeshi la Israel amesema hakukuwa na kifo chochote kilichoripotiwa kufuatia tukio hilo, lakini ameongeza kuwa lau lisingezuiliwa, basi kungetokea maafa.

Waasi wa Kihouthi husema wanafanya mashambulizi yake dhidi ya Israel kuunga mkono Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Mashambulizi ya Alhamisi yanatishia kutanua machafuko kati ya Israel na Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran, ambao mashambulizi yao dhidi ya meli zinazopita bahari ya Shamu yameathiri pakubwa usafirishaji bidhaa kote ulimwenguni.

Jeshi la Israel limesema limefanya mawimbi mawili ya mashambulizi ya angani katika operesheni iliyopangwa awali na iliyoanza mapema Alhamisi. Operesheni hiyo ilihusisha ndege za kivita 14.

Jeshi hilo limesema wimbi la kwanza la mashambulizi lililenga miundombinu ya Wahouthi katika bandari za Hodeida, Salif na kituo cha mafuta cha Ras Isa katika Bahari ya Shamu.

Katika wimbi la pili la mashambulizi, ndege za kivita za Israel zilishambulia miundo mbinu ya nishati iliyoko mji mkuu wa Yemen - Sanaa.

Soma pia: Marekani yashambulia ngome 15 za Wahouthi, Yemen

Shirika la Habari la al-Masirah linalodhibitiwa na Wahouthi limesema baadhi ya mashambulizi yalipiga vituo vya umeme mjini Sanaa. Shirika hilo lilisambaza video zilizoonesha miundombinu hiyo ikichomeka huku wazima moto wakijaribu kupambana na moto huo.

Likimnukuu mwandishi wake katika bandari ya Hodeida, shirika la al- Masirah limesema watu wasiopungua saba wameuawa huko Salif na wawili wameuawa katika kituo cha mafuta cha Ras Isa. Limeongeza kwamba wengine kadhaa walijeruhiwa kwenye mashambulizi hayo.

Jeshi la Israel halikutoa maelezo kamili kuhusu maafa yaliyotokana na mashambulizi hayo yake.

Unaweza kusoma pia: Vyanzo: Mkataba usitishaji wa vita Gaza unakaribia

Msemaji wa jeshi hilo Daniel Hagari alithibitisha kwamba walishambulia miundo mbinu ya nishati na ya bandari aliyodai waasi wamekuwa wakitumia kwa njia mbalimbali zilizochochea hatua hiyo ya kijeshi.

Israel Katz, waziri wa Ulinzi wa Israel, amewashauri viongozi wa Wahouthi kutafakari, kuelewa na wakumbuke kwamba yeyote anayelishambulia taifa la Israel, atashambuliwa pia, na anayeidhuru Israel, naye atadhuriwa mara saba.

JYmen Sanaa 2024 | Wazima moto wakipambana na moto kutokana na mashambulizi ya israel
Miongoni mwa maafa yalkiyotokea ni vifo vya watu tisa na miundombinu ya nishati na bandari kuharibiwa baada ya IUsrael kushambulia vituo mbalimbali nchini Yemen.Picha: Khaled Abdullah/REUTERS

Unaweza pia kusoma: Marekani imefanya mashambulizi ya anga dhidi ya waasi wa Kihouthi Yemen

Kwa muda wa muongo mmoja ambao Yemen imegubikwa na machafuko, Hodeida, mji unaoshikiliwa na waasi na uliopo takriban kilomita 145 kusini magharibi mwa Sanaa, umekuwa muhimu kwa usafirishaji wa chakula kuingia Yemen

Kuna pia wasiwasi wa muda mrefu kwamba silaha kutoka Iran zimekuwa zikiingizwa nchini Yemen kupitia mji huo wa bandari, Hodeida.

Kulingana na afisa wa kijeshi wa Israel, tangu Oktoba 7, 2023, Wahouthi wamerusha zaidi ya makombora 200 pamoja na zana nyingine za angani dhidi ya Israel.

Tangu mzozo wa Israel dhidi ya wanamgambo wa Hamas ulipoanza, Wahouthi wa Yemen wameshambulia takriban meli 100 za kibiashara kwa makombora na droni.

Israel ilianza vita dhidi ya wanamgambo wa Hamas baada ya wanamgambo hao kushambulia kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7, 2023 na kuua watu 1,200 na kushika 250 mateka.

Israel, Marekani na Umoja wa Ulaya huliorodhesha Hamas kuwa kundi la kigaidi.

(APE, DPAE)