Jaji Barrett ndio chaguo la Trump nafasi ya Mahakama Kuu
27 Septemba 2020"Leo nina furaha kumteua mmoja wa watu wenye busara na mwenye kipawa cha sheria katika mahakama kuu", amesema Trump katika hafla rasmi iliyofanyika Ikulu ya White House. "Ni mwanamke mwenye mafanikio yasiyo na kifani, akili kubwa, sifa nzuri na uaminifu thabiti kwa katiba".
Trump alitarajiwa kwa kiasi kikubwa kumteua Barrett mwenye umri wa miaka 48 na Jaji wa mahakama ya rufaa aliyeteuliwa na Trump na ambaye pia alikuwa chaguo la Republican kutokana na misimamo yake ya nyuma kuhusu masuala ya utoaji mimba, haki za matumizi ya silaha na uhamiaji.
Kifo cha Jaji Ginsburg siku nane zilizopita akiwa na umri wa miaka 87, kiliamsha mjadala mkali juu ya kubadilishwa kwake katika mahakama ya juu. Republican walishinikiza mabadiliko ya haraka ya jaji wa mahakama kuu wakitarajia kutumia wingi wao katika bunge la seneti na udhibiti wa Ikulu.
Wateule wa mahakama kuu kuidhinishwa na Seneti
Kulingana na taratibu, wateule wa mahakama ya juu ni lazima waidhinishwe kwa wingi wa kura katika bunge la Seneti ambalo kwa hivi sasa linadhibitiwa na Republican. Kiongozi wa walio wengi katika Seneti Mitch McConnell, amemmwagia sifa Barrett kama "mteule aliyekidhi vigezo", kauli ambayo imedhihirisha wazi kwamba bunge hilo litapitisha chaguo la Trump.
Seneta wa Republican Lindsey Graham ambaye anaongoza kamati ya bunge ya masuala ya mahakama amekieleza kituo cha Fox News kwamba mchakato wa kumuidhinisha utaanza Oktoba 12.
Wakati huo Democratic wanajaribu kuchelewesha uamuzi huo, licha ya kwamba wanayo mamlaka kidogo ya kimchakato. Wanadai kuwa mshindi wa urais wa Novemba 3 ndiye anapaswa kuamua uteuzi huo wa kudumu katika mahakama iliyo na majaji tisa. Waliberali wana hofu ya mabadiliko ya kiitikadi na kifalsafa katika mahakama hiyo, ambayo yatachangia mageuzi katika masuala ya huduma ya afya, utoaji mimba na kufuatilia mamlaka ya serikali iliyo madarakani.
Ikiwa ataidhinishwa, Barrett anahofiwa kuondoa haki za utoaji mimba pamoja na kubatilisha mpango wa huduma ya afya uliopitishwa na rais mstaafu Barack Obama. Katika kauli yake mgombea wa urais wa Democratic Joe Biden amesema "Seneti halipaswi kushughulikia nafasi hii hadi pale Wamarekani watakapochagua rais na bunge jipya".
Barrett, mama wa watoto saba kutoka Louisiana na Mkatoliki anaonekana kuwa na itikadi tofauti za jaji aliyemtangulia. Katika hafla ya uteuzi wake Barret amesema "atamkumbuka mtangulizi wake". Pia ameongeza kuwa atafuata mkondo wa jaji wa zamani wa mahakama ya juu Antonin Scalia, akisema "jaji ni lazima afuate sheria kama ilivyoandikwa. Majaji sio watunga sera".
Vyanzo: DPA/Reuters