1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatua kali zitachukuliwa kwa wanaokiuka mkataba wa amani

7 Februari 2020

Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Faustin Archange Touadera amewataka washirika wa kimataifa kuchukua msimamo mkali dhidi ya makundi yenye silaha ambayo yanakiuka masharti ya makubaliano ya amani.

https://p.dw.com/p/3XOyc
Zentralafrikanische Republik Parteitreffen mit Präsident Touadera
Picha: DW/J. M. Bares

Mwaka uliopita, serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ilisaini mpango wa kusitisha mapigano na makundi 14 ya waasi, lakini zaidi ya theluthi mbili ya eneo la nchi hiyo bado linadhibitiwa na makundi yenye silaha.

Rais Touadera ameutaka Umoja wa Afrika pamoja na jumuiya ya ushirikiano wa kiuchumi wa nchi za Afrika ya Kati, ECCAS kufafanua kuhusu vikwazo vinavyowezekana dhidi ya makundi ya waasi ambayo yanaukiuka mkataba huo.

Kifungu cha 35 cha mkataba huo wa amani kinaruhusu vikwazo dhidi ya watu wanaokiuka makubaliano, lakini maelezo kuhusu hatua za kuchukuliwa hayajatolewa.

Siku ya Jumatano, shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty International liliyaonya makundi kadhaa yenye silaha ambayo bado yanaendeleza ukatili dhidi ya raia, ikiwemo kufanya mauaji na unyanyasaji wa kingono, licha ya kusaini makubaliano.

Chanzo: afp