Jaribio la kombora la Korea kaskazini lashindwa
16 Aprili 2017Kushindwa huko , ambako kunaonekana kwa umma kama kitu cha fadhaa kwa serikali ya nchi hiyo, kumekuja huku hali ya wasi wasi ikiongezeka katika kanda hiyo kuhusiana na dhamira ya Korea kaskazini kujipatia silaha za kinyuklia.
"kombora hilo liliripuka mara moja," wizara ya ulinzi ya Marekani ilisema kuhusiana na jaribio hilo lililofanywa mapema leo asubuhi ambalo taarifa zake zilipatikana kupitia jeshi la Korea kusini. Hata hivyo haikuwezekana kufahamu mara moja ni aina gani ya kombora lilitumika katika jaribio hilo, muda ambao unaonekana kuwa uliamuliwa kwa makusudi kabisa.
Jaribio hilo limekuwa baada ya Korea kaskazini kuonesha karibu makombora 60 , ikiwa ni pamoja na kile kinachoshukiwa kuwa kombora jipya linaloweza kuvuka mabara , katika gwaride siku ya Jumamosi kuadhimisha miaka 105 ya kuzaliwa kwa muasisi wa taifa hilo Kim II-Sung.
Sherehe hizo zilifanyika mbele ya kamera za mashirika ya habari duniani yaliyoalikwa, ambayo yalikuwapo pia Pyongyang wakati wa jaribio la kurusha kombora hilo lililoshindwa. Kushindwa kwa kombora hilo kurushwa kunakuja masaa machache kabla ya ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence nchini Korea Kusini ambako mpango wa silaha wa taifa hilo lililoko upande wa kaskazini utakuwa ajenda ya juu.
Tabia ya ukaidi
Korea Kaskazini ina tabia ya kurusha makombora kuadhimisha sherehe muhimu za kisiasa, ama kama ishara ya ukaidi mnamo wakati maafisa wa ngazi ya juu wa Marekani wanapofanya ziara katika eneo hilo.
Waziri wa ulinzi wa Marekani Jim Mattis amesema Trump amefahamishwa kuhusu jaribio hilo la hivi karibuni lakini "hakutoa maelezo zaidi".
Tukio la leo Jumapili la kurushwa kwa kombora kumefanyika majira ya alfajiri kutoka Sinpo , eneo la kurushia makombora upande wa pwani ya mashariki ya Korea kaskazini ambako nchi hiyo ina eneo la kuegesha meli.
Mwezi Agosti mwaka jana, kombora lililorushwa kutoka katika nyambizi kutoka Sinpo liliruka kilometa 500 kuelekea Japan. Kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong-Un amesifu jaribio hilo kuwa "ni mafanikio makubwa" na kusema limeiweka Marekani kuwa karibu na mfumo wa kurusha makombora unaoweza kuhamishika.
Trump hajasema lolote
Rais Trump amesema mara kadhaa atazuwia Pyongyang kufikia lengo lake la kutengeneza makombora yenye silaha za nyuklia yanayoweza kufika nchini Marekani.
Huku uvumi ukiongezeka kuwa Korea kaskazini inajitayarisha kufanya jaribio la sita la makombora ya nyuklia ametuma meli ya kivita yenye ndege za kivita katika rasi ya Korea--ishara ya wazi baada ya Marekani kufanya shambulio la makombora nchini Syria.
Korea kaskazini imerudia matamshi yake ya kila wakati kwamba iko tayari kwa "vita" na Marekani , na Jeshi lake limeapa siku ya Ijumaa kujibu "bila huruma" uchokozi wa aina yoyote kutoka Marekani.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Caro Robi