Je chanjo ya AstraZeneca ni salama?
8 Aprili 2021Utata na mashaka bado unazidi kujitokeza kuhusu chanjo dhidi ya virusi vya Corona ya AstraZeneca. Nchi mbali mbali za ulimwengu zinaonesha mashaka kuelekea chanjo hiyo.
Kwanza ifahamike kwamba chanjo ya AstraZeneca imedhaminiwa na Uingereza na shirika la afya duniani WHO bado linaiunga mkono chanjo hiyo likisema licha ya madai yanayotolewa ya kuihusisha chanjo hiyo na athari ya damu kuganda yanaonesha kuwa na uwezekano wa kuingia akilini kwa mujibu wa data,lakini ni suala ambalo halijathibitika.
Taasisi ya kudhibiti na kufuatilia usalama wa dawa barani Ulaya EMA mwanzoni kabisa ilithibitisha mapendekezo yake juu ya matumizi ya chanjo hiyo kwa watu wazima lakini pia lilisisitiza kwamba tatizo la damu kuganda liorodheshwe kama moja ya athari ya nadra sana inayoweza kusababishwa na chanjo hiyo.
Taasisi hiyo ya kusimamia dawa Ulaya EMA iliidhinisha chanjo ya Astra Zeneca pamoja na chuo kikuu cha Oxford mnamo mwezi Januari lakini utolewaji wa chanjo hiyo katika nchi nyingi za Ulaya ni wa mashaka huku baadhi ziweka sheria zao kuhusu nani anapaswa kudungwa chanjo hiyo na nani hapaswi,lakini wakati mwingine pia nchi hizohizo zinabadili mkondo.
Msimamo wa nchi za Umoja wa Ulaya
Tukianzia hapa Ujerumani kwa hivi sasa nchi hiyo imeamua wanaodungwa chanjo hiyo ni wazee wa umri wa zaidi ya miaka 60 kama ilivyoamua pia Uhispania. Ubelgiji imetangaza jana jumatano itasitisha kwa muda kutoa chanjo hiyo kwa watu wote wenye umri wa miaka 55 na kwenda chini kama ambavyo pia inafanya Ufaransa. Nchi nyingine za Umoja wa Ulaya zimesitisha kabisa utoaji wa chanjo hiyo tangu katikati ya mwezi March na bado hazijaruhusu itumike.
Lakini kwa upande taasisi za kusimamia masuala ya afya nchini Uingereza,ambayo sio tena mwanachama wa Umoja wa Ulaya,jana ziliruhusu chanjo hiyo idungwe watu wenye umri wa zaidi ya miaka 30 baada ya maafisa kwa wiki kadhaa kusisitiza kwamba hakuna haja ya kuweka vikwazo katika matumizi ya chanjo hiyo.
Taasisi ya Afrika ya kudhibiti magonjwa AfricaCDC kupitia mkuu wake John Nkengasong imesema bado itaendelea kusambaza chanjo ya Astrazeneca katika nchi za bara hilo kupitoa mpango wa kugawa chanjo kwa nchi masikini COVAX.Ingawa Umoja wa Afrika utaagiza chanjo ya ziada kutoka kampuni ya Johnson&Johnson. Barani Asia Korea Kusini maafisa wa afya wameeleza kwamba watatoa uamuzi wao mwisho wa juma hili juu ya ikiwa wataruhusu chanjo hiyo kwa watu wa zaidi ya umri wa miaka 60 na vijana au la.Ufilipino nayo leo imesimamisha kabisa matumizi ya chanjo hiyo ya Astrazeneca kwa watu chini ya umri wa miaka 60 kufuatia ripoti kutoka nje kuhusu chanjo hiyo kusababisha damu kuganda. Nchi hiyo kufikia sasa imepokea dosi milioni 2.5 ya chanjo na serikali hiyo ya mjini Manila imekuwa kwenye mazungumzo na watengenezaji 7 wa chanjo. Lakini pia serikali ya Ufilipino imesisitiza kwamba kusimamishwa kwa muda chanjo hiyo haimaanishi kwamba sio salama.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri: Josephat Charo