Je, ni kwa nini kundi la BRICS linaipinga sarafu ya dola?
5 Desemba 2024Jina la BRICS linatokana na nchi waanzilishi wa jumuiya hiyo ambazo ni Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini. Jumuiya hiyo ya BRICS, imeongeza idadi ya wanachama wake baada ya nchi za Iran, Misri, Ethiopia na Falme za Kiarabu kujiunga nayo hivi karibuni.
Wanachama hao wa BRICS wanailaumu Marekani kwa kutumia sarafu yake ya dola kama silaha kwa kuzilazimisha nchi zizonaipinga Marekani kuendesha miamala katika mfumo unaozingatia na kulinda maslahi ya Marekani.
Soma pia:Putin asema Marekani itaamua yenyewe uhusiano baina yao
Wataalamu wengi wa maswala ya uchumi wanakubaliana kwamba mfumo wa kifedha unaotawaliwa na dola huipa Marekani faida kuu za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na gharama za chini za kukopa, uwezo wa kudhibiti nakisi kubwa ya fedha na uthabiti wa viwango vya ubadilishaji fedha, miongoni mwa mambo mengine.
Dola hutumiwa kupanga bei za bidhaa muhimu
Dola ndiyo sarafu kuu inayotumiwa kupanga bei za bidhaa kama vile mafuta na dhahabu na uthabiti wake unamaanisha kuwa wawekezaji mara nyingi huchagua kutumia dola hata katika nyakati zisizo na uhakika kwenye masoko.
Marekani pia inanufaika kutokana na ushawishi mkubwa wa siasa za kikanda kutokana na kile kinachoitwa uimara wa sarafu ya dola, ikiwa ni pamoja na kuipa uwezo nchi hiyo wa kuweka vikwazo kwa mataifa mengine na kuyazuia kushiriki kwenye masoko ya biashara na mitaji.
Soma pia: BRICS: Putin asema kuishinda Urusi ni ndoto isiyofikirika
Majadiliano kuhusu kuanzishwa sarafu mpya ya pamoja yalipata nguvu baada ya Marekani na Umoja wa Ulaya kuiwekea Urusi vikwazo kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine mnamo mwaka 2022. Mataifa mengine wanachama wa BRICS yalipata wasiwasi kwamba pia yanaweza kulengwa iwapo yatatofautiana na nchi za Magharibi.
Katika mkutano wa BRICS wa mwaka jana nchini Afrika Kusini, jumuiya hiyo ilikubali kuangalia uwezekano wa kuunda sarafu ya pamoja ili kupunguza uwezekano wa hatari zinazoweza kusababishwa na dola, ingawa viongozi wa BRICS walibainisha kuwa huenda itachukua miaka mingi jambo hilo kutekelezwa.
Rais Putin na mwenzake wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva ndio wafuasi wakuu wa sarafu hiyo mpya. Ingawa China haijatoa maoni kwa uwazi, lakini serikali imesema inaunga mkono juhudi za kupunguza utegemezi wa dola.
Je! Kitisho cha Rais mteule wa Marekani Donald Trump cha kuweka ushuru kwa asilimia 100 amekitoa mapema mno?
Trump aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii Truth Social, kwamba atakaporejea ikulu ya Marekani mwezi Januari, atazitaka nchi wanachama wa jumuiya ya BRICS kutoa hakikisho kwamba hazitaunda sarafu mpya ya BRICS au kuanzisha sarafu nyingine yoyote kwa nia ya kuchukua nafasi ya dola ya Marekani.
Hata hivyo Rais huyo mteule wa Marekani, huwenda ameharakisha kwa kiasi fulani kulizungumzia hilo kwa sababu pendekezo la kuanzishwa sarafu ya BRICS halijapiga hatua zozote licha ya matamshi kutoka kwa viongozi wa BRICS amesema Chrispin Phiri, msemaji wa Idara ya uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano nchini Afrika Kusini,
Amesema amesema pamoja na vitisho vya Trump vya kutoza ushuru wa ziada kwa wapinzani wa Marekani, ikiwa ni pamoja na China, hatua hiyo inaweza kuongeza mfumuko wa bei duniani na ndani, na hivyo kuathiri ukuaji wa uchumi wa Marekani.
Msemaji wa serikali ya Urusi Dmitry Peskov, alisema hali inazidi kushika kasi kupinga kutumiwa dola kama sarafu ya akiba, akisema kuwa nchi zaidi zinaunga mkono matumizi ya fedha zao za kitaifa katika biashara na shughuli za kiuchumi za kimataifa.