Je, ongezeko la udhibiti wa mipaka linazima ndoto ya EU?
15 Desemba 2024Mwezi Juni 2025, kijiji cha Schengen kilichopo kusini magharibi mwa taifa dogo la Umoja wa Ulaya, Luxemburg, kitakuwa mwenyeji wa sherehe kubwa. Ilikuwa huko Schengen mnamo Juni 14, 1985, ambapo mawaziri kutoka Uholanzi, Ubelgiji, Luxemburg, Ufaransa na Ujerumani walisaini makubaliano yaliyoweka msingi wa kuvuka mipaka kati ya nchi zao bila ukaguzi wa vitambulisho.
Huu ulikuwa mwanzo wa kile kinachojulikana sasa kama Eneo la Schengen, ambalo kwa sasa linahusisha nchi 25 za Umoja wa Ulaya, pamoja na mataifa yasiyo wanachama wa Umoja wa Ulaya kama Norway, Uswisi, Iceland na Liechtenstein.
Uhuru wa kusafiri ambao raia wengi wa Ulaya wanaufurahia leo mara nyingi huelezewa na Tume ya Ulaya kama moja ya tunu za utangamano wa Ulaya. Hata hivyo, tunu hii inaanza kupoteza mvuto wake.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Luxemburg, Leon Gloden, anayakosoa mataifa ya Schengen ambayo yameanzisha tena ukaguzi wa mipakani kufuatia idadi kubwa ya wahamiaji.
"Hili halikubaliki kwa Luxemburg,” Gloden alisema katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya mnano Desemba 12, 2024. "Schengen ni moja ya mafanikio makubwa ya EU. Hatuwezi kuruhusu mipaka ijengeke tena akilini mwa watu.”
Udhibiti zaidi kuliko wakati mwingine wowote
Mwaka 2024 umeshuhudia ukaguzi mkubwa zaidi wa mipaka ya ndani kuliko wakati mwingine wowote tangu Eneo la Schengen lilipoanzishwa.
Ujerumani imeanzisha tena ukaguzi katika mipaka yake yote ya ardhi na majirani zake tisa kwa mara ya kwanza tangu kuwa mwanachama wa Schengen. Tayari kulikuwa na udhibiti katika mpaka wake wa kusini na Austria tangu mwaka 2015, ili kuzuia wahamiaji wanaofika kupitia njia ya Balkan.
Soma pia: Mkataba wa Schengen huenda ukasimamishwa kwa muda
Ufaransa pia ilianzisha tena ukaguzi wa mipaka mwaka 2015, ikitaja sababu za ugaidi, lakini imekuwa ikiutekeleza kwa vipindi fulani tu.
Nchi nyingi zinazotekeleza ukaguzi zinafanya hivyo tu katika sehemu fulani za mipaka yao. Wageni wasio na nyaraka halali, au wale waliopo kwenye marufuku ya kuingia kutokana na ukiukwaji uliopita, hurudishwa nyuma katika mipaka ya ndani.
Mtu yeyote anayewasilishwa ombi la ukimbizi mpakani anaruhusiwa kuingia kwa muda, kisha hupelekwa katika kituo cha mapokezi cha awali. Sheria ya Umoja wa Ulaya hairuhusu wanachama kuwazuia wote wanaotafuta hifadhi.
Mnamo Desemba 9, 2024, Uholanzi pia ilianzisha udhibiti wa mipaka kwa wasafiri wanaoingia kutoka Ujerumani na Ubelgiji.
Karibu wakati huo huo, mawaziri wa mambo ya ndani wa EU walikubaliana kwamba Romania na Bulgaria zitakuwa wanachama kamili wa Eneo la Schengen kuanzia Januari 1, 2025.
Hivyo, ukaguzi katika mipaka ya ardhini kuelekea nchi hizo mbili za kusini-mashariki mwa Umoja wa Ulaya utaondolewa. Ukaguzi katika viwanja vya ndege kwa safari za ndani ya EU uliondolewa mwaka jana.
Wakati hali ya kipekee inapogeuka utaratibu
Bunge la Ulaya na Tume ya Ulaya husisitiza mara kwa mara kwamba ukaguzi wa kitambulisho katika mipaka ya ndani ya Eneo la Schengen lazima uwe "jambo la kipekee na utumike tu kama "njia ya mwisho.”
Hata hivyo, kila nchi mwanachama inaweza kuanzisha ukaguzi wa mipaka kwa muda wa hadi miezi sita, iwapo itatoa sababu halali kwa Tume ya Ulaya. Ukaguzi huu unaweza kurefushwa kwa muda wa hadi miaka miwili au, katika hali zisizo za kawaida, miaka mitatu.
Soma pia:Wasafirishaji watu, ni marafiki hatari wasiojali maisha
Baada ya hapo, sababu inapaswa kubadilishwa. Hii mara nyingi inahitaji ubunifu fulani. Hadi sasa, Tume ya Ulaya haijaanzisha taratibu zozote rasmi za ukiukwaji wa kanuni za mipaka za Schengen, lakini baadhi ya nchi zimeweka udhibiti kwa muda wa hadi miaka 10.
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Nancy Faeser, alitangaza kuwa ukaguzi kamili katika mipaka yote ya Ujerumani utaendelea kwa muda usiojulikana, hadi idadi ya wahamiaji wanaoingia itakapopungua hadi kiwango fulani kisichotajwa.
"Kadiri idadi ya wanaoingia Ujerumani inavyosalia juu, ndivyo ukaguzi utakavyoendelea,” alisema. "Eneo la Schengen ni muhimu sana kwa Ujerumani, lakini tunahitaji pia ugawaji bora wa wakimbizi.”
Alikuwa akimaanisha utaratibu wa ugawanaji wakimbizi wa Umoja wa Ulaya, ambao unasisitiza kwamba watafuta hifadhi na wakimbizi wapokelewe na nchi ambazo walingia nazo kwanza ndani ya Umoja wa Ulaya.
Lakini kiuhalisia, hili halitokei. Wahamiaji wengi huendelea na safari yao kutoka Ugiriki, Italia, Kroatia au Hispania kwenda nchi za kaskazini za EU kama Ujerumani.
Athari za udhibiti ni zipi?
Athari halisi za ukaguzi wa mipaka ndani ya Eneo la Schengen ni suala la mjadala. Takwimu za polisi ya Ujerumani, ambao hutumia maafisa wapatao 11,000, zinaonyesha kwamba makumi ya maelfu ya watu hujaribu kuingia bila ruhusa, huku takriban nusu wakirudishwa hapo hapo. Nusu nyingine huomba hifadhi. Wanadai kuwa walanguzi wa watu wamekamatwa, na maelfu ya hati za kukamatwa zimetekelezwa.
Hata hivyo, chama cha polisi cha Ujerumani (GDP) kinakadiria kwamba idadi halisi ya wanaoingia bila ruhusa na wanaorudishwa ni ndogo zaidi. Aidha, kama anavyoeleza mkuu wa chama hicho, Andreas Rosskopf, ukaguzi unaweza kufanyika tu katika sehemu maalum kwenye barabara kubwa. Hata hivyo, Ujerumani ina mpaka wenye urefu wa kilomita 7,000 na mtandao mkubwa wa barabara na reli unaounganisha na nchi jirani.
Soma pia: Jean-Claude atoa wito kukomeshwa kwa ukaguzi wa mpaka katika Umoja wa Ulaya
Polisi hukagua sehemu ndogo tu ya watu wanaoingia nchini kwa gari au treni. Wamepewa maagizo mahsusi na wizara ya mambo ya ndani kufanya ukaguzi wa kushtukiza tu, ili kuepuka foleni kubwa za magari.
Rosskopf aliuambia mtandao wa habari wa Ujerumani (RND) kwamba mabasi ya masafa marefu yanayotoka kusini mwa Ulaya wakati mwingine husimamishwa barabarani (Autobahn), lakini madereva wengi wa basi sasa wamezoea maeneo yanayoweza kuwa na ukaguzi na hutumia barabara ndogo kukwepa.
‘Hisia ya usalama'
Kamishna mpya wa masuala ya ndani na uhamiaji wa Umoja wa Ulaya, Magnus Brunner kutoka Austria, ambaye pia anawajibika kwa Eneo la Schengen, alionyesha kuelewa kuongezeka kwa udhibiti wa mipaka.
"Tunahitaji kuboresha usalama ndani ya eneo la Ulaya,” alisema. "Lakini tunapaswa kufuata matakwa ya kisheria. Tunahitaji kufanya kazi ya kuboresha ulinzi wa mipaka ya nje, ili kuwapa watu hisia kwamba tunadhibiti tena ni nani anayeingia.”
Ni vigumu kujua ikiwa hili litatimia kabla ya maadhimisho ya miaka 40 ya makubaliano ya Schengen mwaka 2025.
Hata hivyo, Luxemburg bado inapanga kusherehekea "mahali palipozaliwa Ulaya isiyo na mipaka,” kama a,bavyo Schengen inapenda kujiita, Juni ijayo.