1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jean-Pierre Bemba arejea DRC kuwania urais

1 Agosti 2018

Kiongozi wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Jean-Pierre Bemba, amerejea nyumbani Jumatano baada ya muongo mzima gerezani mjini The Hague, kuwania urais katika uchaguzi wa Desemba.

https://p.dw.com/p/32Ro2
Kongo Ankunft Oppositionsführer Jean-Pierre Bemba
Picha: Reuters/J. R. N'Kengo

Bemba ambaye hukumu yake ya uhalifu wa kivita katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ilibatilishwa Mei, aliwasili katika uwanja wa ndege wa N'Djili mjini Kinshasa, ambako maelfu y wafuasi wake walikuwa wakimsubiri wakivalia fulana, kofia, skafu na vitambaa vyenye sura yake.

Akivalia suti nyeusi na tai nyekundu, Bemba mwenye umri wa miaka 55 alishikana mikono na wanafamilia na maafisa kutoka chama chake cha MLC kabla ya kupanda gari kuelekea mjini kati ambako alitarajiwa kuhudhiria misa.

Afisa wa chama cha MLC Jean-Jacques Mbungani aliwaambia waandishi kuwa Bemba atawasilisha maombi yake ya kugombea kwa tume ya uchaguzi siku ya Alhamisi kabla ya kusafiri kuelekea mji wake wa nyumbani wa Gemena kaskazini-magharibi mwa Congo kutoa heshima kwa hayati baba yake.

"Watu wa Congo wamesubiri wakati huu kwa muda mrefu," alisema Toussaint Bodongo, afisa wa MLC. "Pengine Bemba ataleta suluhisho la kile tunachokihitaji nchini Congo."

Kongo Ankunft Oppositionsführer Jean-Pierre Bemba
Bemba alipopokelewa na maafisa wa juu kutoka chama chake cha MLC katika uwanja wa ndege wa N'Djili mjini Kinshasa.Picha: Reuters/J. R. N'Kengo

Kurejea kwa makamu huyo wa zamani wa rais na mbabe wa kivita kunatazamiwa kuutia hamasa upinzani dhidi ya Kabila, ambaye amekuwa madarakani tangu kuuliwa kwa baba yake mwaka 2001, na sasa anazuwiwa kikatiba kuwania muhula mwingine kutokana na sheria ya ukomo wa mihula.

Kabila amekataa kusema hadharani kuwa hatowania katika uchaguzi huo. Hatua hiyo imeiweka nchi katika wasiwasi kuhusiana na iwapo atateuwa mtu mwingine kuwakilisha muungano wake tawala, na kusafisha njia kwa mabadiliko ya kwanza ya kidemokrasia nchini Congo, au atarajibu kugombea tena na kuweka hatari ya upinzani wa vurugu.

Vikosi vya usalama vimeuwa fazeni kadhaa za waandamanaji tangu mwishoni mwa mwaka 2016 wakati Kabila alipkataa kuachia madaraka mwishoni mwa muhula wake kikatiba, akisema uchaguzi ulihitaji muda zaidi kuandaliwa. Vurugu za wanamgambo mashariki mwa nchi hiyo zimeongezeka tangu wakati huo.

Vigezo vya kugombea?

Muda wa mwisho kwa wagombea ni Agosti 8. Bemba alisema wiki iliyopita kwamba anaamini yeye ndiye mgombea mwenye nguvu zaidi kuweza kuwakilisha upinzani lakini atakuwa tayari kuachia nafasi yake kwa mgombea mwingine.

Huenda azma yake ya kuogmbea ikapingwa mahakamani. muungano tawala ulisema wiki iliyopita kwamba hana vigezo vya kugombea baada ya kutiwa hatiani kwa mashitaka ya kuingilia ushahidi na mahakama ya ICC hata kama hatia yake ya mauaji, ubakaji na uharibu vilivyofanywa na wapiganaji wake nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 2002 ilitupiliwa mbali.

Kongo Ankunft Oppositionsführer Jean-Pierre Bemba
Wafuasi wa Bemba wakijipanga barabarani kumpokea.Picha: Reuters/K. Katombe

Kubatilishwa kwa ugombea wa Bebmba kunaweza kuwakasirisha wafuasi wake, hasa magharibi mwa Congo. Kushindwa kwake na Kabila mwakak 2006 kulipelekea mapambano ya silaha katika mitaa ya mji mkuu Kinshasa kati ya wapiganaji wake na wanajeshi wa serikali.

"Watakapojaribu kumuweka kando, tunajua hiyo itakuwa siasa," alisema Denis Vila, mratibu wa mkoa wa tawi la wanawake la chama cha MLC. "Tutapigana ili Jean-Pierre bemba abakie katika kinyanganyiro hicho."

Mgombea mwingine wa upinzani, mfanyabiashara tajiri na mkuu wa zamani wa mkoa Moise Katumbi, pia anapanga kurejea nchini Congo siku ya Ijumaa baada ya miaka miwili uhamishoni lakini ana hatari ya kukamatwa kutokana na kutiwa hatiani kwa udanganyifu unaohusiana na umiliki wa majumba mwaka 2016.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliochapishwa siku ya Jumanne, Katumbi na kiongozi mwenzake wa upinzani, Felix Tshisekedi, anaongoza kinyanganyiro cha urais kila moja akiwa na asilimia 19. Bemba angepata asilimia 17 na Kabila asilimia tisa.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre

Mhariri: Mohammed Khelef