Suluhisho la Waafrika kwa matatizo ya Afrika
19 Oktoba 2015Bara la Afrika lilikuwa linataka kuchukua jukumu la kutatua matatizo yake binafsi. Je jeshi hili linaweza kweli kutimiza matarajio ya watu wa bara hilo.
Tangu mwaka 2003 kulikuwa na majadiliano ya kuunda jeshi la kudumu la bara la Afrika , ambalo lingeweza kutumwa katika maeneo mbali mbali ya vita, litakalojulikana kama „ jeshi la Afrika lililo tayari“, ama „African Standby Force“ kwa ufupi ASF.
Kwa miaka mitano iliyopita jeshi hilo limekuwa likitayarishwa, lakini kumekuwa na hali ya kukatisha tamaa. Lakini hatimaye sasa hatua zinachukuliwa na leo tarehe 19, Oktoba yanaanza rasmi nchini Afrika kusini mafunzo kwa ajili ya jeshi hilo.
Kwa miaka 12 iliyopita jeshi hilo limekuwa likipangwa na kujadiliwa tu, na baada ya kuahirishwa mara kadhaa sasa muda uliowekwa kuzinduliwa rasmi jeshi hilo ni Desemba , 2015.
Jeshi la vikosi vitano
Hadi wakati huo jeshi hilo litakuwa linafanya luteka. Jeshi la Afrika lililoko tayari, litakuwa na wanajeshi 25,000 na kujenga msingi wa mfumo wa usalama na amani katika bara la Afrika . Jeshi hilo litaundwa na vikosi vitano. Wanajeshi wa jeshi hilo watapatikana kutoka jumuiya tano za kiuchumi katika bara la Afrika.
Teferra Shiawl-Kidanekal, mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya utafiti endelevu mjini Addis Ababa na mtaalamu wa siku nyingi wa sera za usalama katika bara la Afrika, anafafanua kuhusu wazo la kuwa na jeshi hilo.
Tuna baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika ambalo limeamua kutuma wanajeshi wa kulinda amani katika hali kama ya nchi ya Somalia. Wakati huo huo tunalitayarishaje jeshi hilo kwa ajili ya kufanya kazi hiyo? Umoja wa Afrika umekuwa na mfumo huu wa jeshi litakalokuwa tayari.
Amani Afrika mbili
Jeshi hili linaundwa na vikosi kutoka jumuiya tano za kiuchumi barani Afrika, ECOMOG ya Afrika magharibi, SADC ya kusini mwa Afrika, ESF ya Afrika mashariki na NARC ya Afrika kaskazini.
Leo Jumatatu(19.10.2015) jeshi hilo la bara la Afrika litakusanyika kwa mara ya kwanza katika eneo la mazowezi. Na kisha jeshi hilo litaanza rasmi luteka ya pamoja nchini Afrika kusini. Hii ina maana kuanza rasmi kwa jeshi hilo,kama anavyoeleza meja jenerali kutoka Nigeria Samaila Iliya wakati akizungumza na DW.
"Mazowezi ya jeshi hilo yatakayojulikana kama (Amani Afrika 2) ni mwanzo wa kuelekea katika jeshi la Afrika litakalokuwa tayari. Baada ya hapo batalioni tofauti zitakuwa tayari kupelekwa wakati wowote katika maeneo ya mizozo kwa idhini ya baraza la usalama na amani la Umoja wa Afrika."
Hadi sasa nadharia hii ya matumaini inaonekana kuchukua mtazamo mwingine kabisa katika hali halisi kimataifa. Umoja wa Mataifa ulikuwa na jeshi kama hilo baada ya miaka 13 na limetumika mara moja tu. Umoja wa Ulaya pia hadi sasa unasubiri kuundwa kwa jeshi kama hilo, anaeleza mtaalamu wa Ujerumani wa masuala ya usalama Sebastian Gräfe.
Mwandishi Ludger Schadomsky / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri: Yusuf Saumu