1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Burkina Faso laahidi kuunda serikali ya umoja

Admin.WagnerD3 Novemba 2014

Jeshi la Burkina Faso limeahidi kuhakikisha serikali ya umoja ipo madarakani baada ya kulidhibiti taifa hilo la magharibi mwa Afrika kwa kujitangaza ndiyo viongozi wa muda na kuwatawanya waandamanaji wanaowapinga

https://p.dw.com/p/1Dfz6
Picha: Issouf Sanogo/AFP/Getty Images

Wanajeshi wa Burkina Faso wameingia katikati ya mji mkuu wa nchi hiyo Ougadogou kuwatawanya waandamanaji kwa kurusha gesi ya kutoa machozi na risasi hewani na kuyadhibiti makao makuu ya kituo cha televisheni cha serikali licha ya wito kutoka kwa jumuiya ya kimataifa na waandamanaji wa kurejeshwa kwa utawala wa kiraia nchini humo.

Jeshi hilo ambalo lilichukua madaraka Ijumaa iliyopita baada ya Rais Blaise Compaore kujiuzulu baada ya kuwa madarakani kwa miaka 27 na kushurutishwa na wananchi kung'atuka uongozini baada ya kujaribu kubadilisha katiba, limeahidi kuunda serikali ya mpito itayoshirikisha kila pande baada ya jumuiya ya kimataifa kutisha kuiwekea Burkina Faso vikwazo vya kiuchumi.

Jeshi lasema halitaki madaraka

Taarifa iliyotolewa na jeshi hilo baada ya kiongozi wa muda Luteni Kanali Isaac Zida kukutana na viongozi wa upinzani imesema hawana nia ya kuchukua madaraka bali wamechukua hatua za kuhakikisha maslahi ya taifa hilo yanazingatiwa hivi sasa.

Kiongozi wa muda wa Burkina Faso Luteni kanali Isaac Zida na kiongozi wa upinzani Diabre
Kiongozi wa muda wa Burkina Faso Luteni kanali Isaac Zida na kiongozi wa upinzani DiabrePicha: Reuters/J. Penney

Balozi wa Umoja wa Mataifa kuhusu magharibi mwa Afrika Mohammed Ibn Chambas amesema ameungana na viongozi wengine wa Afrika kulishinikiza jeshi la Burkina Faso kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.

Wito kama huo pia umetolewa na Marekani na Umoja wa Ulaya.Katika taarifa iliyotolewa hapo jana,Umoja wa Ulaya umelitaka jeshi la Burkina Faso kuheshimu haki za kimsingi za raia ikiwemo uhuru wa kuandamana kwa amani na kuongeza inatumai kuona utawala wa kiraia ukiwepo haraka iwezekanavyo kuandaa mazingira mazuri ya kufanyika uchaguzi huru na wa haki hivi karibuni.

Raia waandamana kulipinga jeshi

Kulingana na katiba ya Burkina Faso,spika wa bunge ndiye alipaswa kuchukua madaraka kwa muda baada ya kujiuzulu kwa rais lakini badala yake jeshi ndilo lilitangaza kuchukua madaraka. Kwanza mkuu wa majeshi Honore Traore alijitangaza kiongozi na siku moja baadaye Zida ambaye ni kamanda wa pili katika kikosi cha ulinzi wa rais akatangaza kuwa yeye ndiye kiongoziwa muda wa taifa hilo.

Raia wakiandamana Ougadogou kupinga jeshi kuwepo madarakani
Raia wakiandamana Ougadogou kupinga jeshi kuwepo madarakaniPicha: Issouf Sanogo/AFP/Getty Images

Hatua hiyo hata hivyo imewaghadhabisha raia wa Burkina Faso ambao walirejea tena barabarani kuandamana wakimtaja Zida kuwa msaliti huku baadhi ya waandamanaji wakielekea katika makao makuu ya kituo cha televisheni ya serikali ambapo viongozi wawili wa upinzani walijaribu kila mmoja kujitangaza kuwa kiongozi wa muda wa nchi hiyo.

Raia mmoja aliuawa karibu na kituo hicho cha televisheni baada ya jeshi kufyatua risasi hewani kuwatawanya waandamanaji.

Compaore ambaye aliingia madarakani mwaka 1987 baada ya mapinduzi ya serikali akiwa na umri wa miaka 36 na kumuondoa madarakani na baadaye kuuawa kwa Rais Thomas Sankara hivi sasa amekimbilia katika nchi jirani ya Cote d´Ivoire pamoja na familia na baadhi ya wapambe wake ambako wamepewa hifadhi katika makaazi ya kifahari ya serikali katika mji wa Yamoussoukro.

Mwandishi:Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman