Jeshi la Congo latangaza matokeo ya vita dhidi ya waasi.
3 Desemba 2019Jeshi linatoa matamko hayo wakati wakaazi wa Beni wakiendelea na mgomo pamoja na maandamano kupinga mauwaji pamoja na kuiomba tume ya Umoja wa mataifa Monusco kuondoka Beni.
Akizungumza na wanahabari katika mji wa Beni, msemaji wa majeshi ya serikali ya Congo Jenerali Richard Kasonga alianza kwa kuwapongeza wanachama wa vuguvugu la Lucha, mashirika ya kiraia pamoja na raia wote wa Beni na kwa jumla raia wa Congo kwa kuliunga mkono jeshi la nchi yao.
Jenerali Kasonga alitumia fursa hiyo kutangaza matokeo ya awali ya operesheni zinazoendelea dhidi ya ADF katika eneo hili "Tumeteka Mayangose, tumewaua wanane kati ya makamanda wakubwa sita wa kundi la kigaidi ADF, na tumewauwa watu hao wagaidi, wanaowauwa watu, wanaosababisha watu kuishi katika hali ya hofu katika eneo hili kubwa la Kivu ya kaskazini. Tuliwauwa ADF themanini, tumewashika pia watu wanaofanya kazi na ADF na tumekuwa tukiwahoji, na kwa kweli wametufafanulia mambo."
Aidha jeshi limetangaza nambari ya simu ambayo wakaazi watakuwa wanapiga bila ya malipo, kwa ajili ya kutowa habari kwa wakati unaofaa kwa jeshi, na hiyo inalenga kuzuia mauwaji yanayoendeshwa na ADF na pia kuzuia raia kujiichukulia sheria mkononi pale wanapowauwa watu wanaodhaniwa kuwa ni ADF katika mji wa Beni.
Na wakati majeshi ya serikali yanakabiliana na ADF katika maeneo ya misitu,makundi ya vijana katika mji wa Beni nayo yanaendelea na maandamano, kuomba tume ya Umoja wa mataifa Monusco kuondoka Beni.
Vijana hao waliwaomba watu wote mjini Beni kutembea bila viatu kwa siku mbili yaani jumatatu na jumanne, ili kufanya tambiko la kuwaomba mababu kuliunga mkono jeshi katika operesheni zinazolenga kuwatokomeza waasi wa ADF.
Tujulishe kuwa, katika maandamano ya jana, waandamanaji wawili waliuawa kwa risasi zinazotajwa kuwa zilifyetuliwa na askari polisi,na askari polisi mmoja kuuawa na waandamanaji, baada ya kumushuku kuwa ndie aliwauwa wenzao. Hali ni ni tulivu kwa sasa katika mji wa Beni na baadhi ya maduka yamefunguliwa huku magari pamoja na pikipiki zikizunguka pia. Hata hivyo, shule bado hazijafunguliwa na bado haijulikani ni lini hasa shule hizo zitafunguliwa.