1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Sudan Kusini latwaa ngome kuu ya waasi

Sylvia Mwehozi
7 Agosti 2017

Jeshi la Sudan Kusini limesema limefanikiwa kuitwaa ngome kuu ya waasi ya Pagak iliyopo karibu na mpaka wa Ethiopia baada ya wiki kadhaa za mapambano makali yaliyowalazimisha maelfu ya raia kukimbia mkoa huo.

https://p.dw.com/p/2hpaa
Südsudan Kämpfer
Picha: picture alliance/AP Photo/J. Lynch

Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini, Dickson Gatluak, amesema vikosi vitiifu vya waasi kwa kiongozi aliyeko uhamishoni na aliyewahi kuwa makamu wa rais, Riek Machar, vimeondoka katika mji huo jana Jumapili bila ya kupigana.

Amesema kumekuwa na machafuko katika mji wa karibu wa Maiwut na vikosi vya serikali vimewasukuma nyuma waasi kuelekea Pagak. Baadaye mchana, waasi walikimbia kutoka mji wa Upper Nile ambao kwa muda mrefu umekuwa ni makao makuu ya wapiganaji wa Machar.

Naye msemaji wa jeshi la waasi la SPLA-IO, Brigedia Jenerali William Gatjiath, amethibitisha kuondoka kwa vikosi vyake katika mji huo lakini akasema kwa hivi sasa wanaudhibiti mji wa Maiwut na wanajitayarisha kuitwaa tena ngome yao. "Kwa hivi sasa tunapozungumza vikosi vyetu vimeizingira Pagak" amesema kamanda huyo.

Südsudan Rebellenführer Riek Machar in Juba
Rais Salva Kiir na Riek Machar wakati akiwa makamu wa raisPicha: Reuters/Stringer

Msemaji wa waasi, Lam Paul Gabriel, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba vikosi vya waasi viliondoka katika eneo hilo la Pagak baada ya kuona kwamba iingewagharimu raia.

Licha ya anguko hilo, Lam anasema haimaanishi ndio mwisho wa mapambano ya kabila la Nuer dhidi ya serikali na vikosi vya Sudan Kusini vinayotawaliwa kwa kiasi kikubwa na kabila la Dinka.

Mchambuzi huru wa Sudan Kusini, Alan Boswell, anasema Pagak imekuwa na umuhimu katika uasi wa Machar katika mgogoro wa kabila lake la Nuer dhidi ya kabila la Rais Kiir la Dinka. "Ni ishara ya pigo kubwa katika harakati za waasi. Pagak imekuwa ni makao makuu tangu kuanza kwa uasi . Kama isingekuwa ni kusambaa kwa vita nchi nzima, hii ingetoa taswira ya kumalizika kwa uasi, " amesema Boswell.

Oppositionsführer Riek Machar bei PK
Kiongozi wa waasi aliyeko uhamishoni Riek MacharPicha: imago/Xinhua

Sudan Kusini ilitumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013 wakati Rais Salva Kiir alipomtuhumu makamu wake wa zamani, Machar, kwa kupanga njama za mapinduzi. Machar alilazimika kukimbilia uhamishoni nchini Afrika Kusini mwishoni mwa mwaka jana, lakini Pagak ilisalia kuwa ngome kuu kwa vikosi vyake tiifu.

Mapema mwaka huu serikali ilitangaza usitishaji wa mapigano wa pamoja lakini ripoti zimeendelea kutolewa kwamba serikali iliendeleza mashambulizi kuelekea miji ya Mewut na Pagak, ikiwemo uchomaji wa nyumba na mauaji ya raia.

Makumi kwa maelfu ya watu wameuawa na wengine mamilioni kulazimika kuyakimbia makaazi yao tangu kuanza kwa mgogoro huo. Takwimu za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa zinasema nusu ya wakazi wa nchi hiyo, wakikadiriwa kufikia milioni sita watahitaji msaada wa chakula cha dharura mwezi huu.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/Reuters/AP

Mhariri: Mohammed Khelef