JOHANNESBURG: Mgomo wa wafanyikazi watatiza shughuli Afrika Kusini
14 Juni 2007Matangazo
Makamu wa Rais wa chama tawala cha ANC, Jacob Zuma, amesema mgomo wa sekta ya utumishi wa umma ambao umekuwa ukiendelea tangu wiki mbili zilizopita nchini Afrika Kusini umeipa sifa mbaya serikali hiyo katika mataifa ya nje.
Jacob Zuma amesema mgomo huo ungeepukwa tangu awali.
Makamu wa rais wa chama cha ANC amesema mashauriano yalioanza tangu Juni mosi wakati mgomo huo ulipoanza, yanaonyesha kuna uwezekano wa serikali kupatana na vyama vya wafanyi kazi.
Sekta ya uchukuzi wa umma, shule, pamoja na hospitali zimeathiriwa kwa kiasi kikubwa tangu mgomo huo ulipoanza kwa lengo la kuishinikiza serikali ikubali nyongeza ya mshahara ya asilimia kumi na mbili.