1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JOHANNESBURG-Rais Gbagbo afurahishwa na makubaliano ya amani ya Afrika Kusini

7 Aprili 2005
https://p.dw.com/p/CFPf

Rais Laurent Gbagbo wa Ivory Coast,ameonesha kuridhishwa baada ya pande zinazohasimiana katika taifa hilo la Afrika Magharibi,kufikia makubaliano ya kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe,huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Kofi Annan akizitaka pande zote kuheshimu makubaliano waliyofikia.

Akizungumza mjini Abijan akiwa anataokea Pretoria,Afrika Kusini,baada ya mkutano wa siku nne wa usuluhishi uliosimamiwa na Rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki,Rais Gbagbo amesema amefurahishwa na makubaliano hayo ambayo yanataka pande zote kuacha kushambuliana na pia kupangwa tarehe ya kufanyika uchaguzi mkuu mwezi wa Oktoba.

Viongozi watano wa Ivory Coast jana waliahidi kuiweka nchi yao katika mstari wa kuelekea amani,kwa kuweka silaha chini,kutatua mzozo wa nani anayefaa kuwa mgombea urais na kuweka mazingira mazuri yatakayowaingiza waasi ndani ya serikali ya umoja.

Kipengele ambacho Rais Gbagbo amesema bado kinautata ndani ya katiba,ni mgombea urais kuwa wazazi wake wote wawili ni lazima wawe raia wa Ivory Coast.Kipengele hicho bado hakijapatiwa ufumbuzi katika mkutano huo wa usuluhishi na rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini amesema atawasiliana na viongozi wa Umoja wa Afrika pamoja na Umoja wa Mataifa,kukipatia ufumbuzi kipengele hicho na kuahidi uamuzi utafikiwa chini ya kipindi cha wiki moja.