Kabila alaumu majeshi ya nje kwa vurugu za DRC
30 Juni 2012Hata hivyo Rwanda imekwisha kanusha madai kwamba inalisaida jeshi lililoasi la waasi wa zamani wenye asili ya Kitutsi ambao kwa hivi sasa wanajulikana kama M23 ambao waliijuinga na jeshi la DRC na baadae kuasi.
Akizungumza katika televisheni ya serikali ,rais Kabila alisema sherehe za uhuru wa Kongo, zinakugubikwa na vitendo vya uasi vinavyofanywa na wapiganaji wa waasi pamoja na wapiganaji kutoka nje ya taifa hilo.
Amesema vitendo hivyo vimeleta machafuko katika eneo la Kivu ya Kaskazini na kusababisha maelfu ya raia kuteseka na kutokuwa na usalama. Kutokana na hali hiyo rais Kabila amesema kuimarisha usalama katika eneo hilo ni suala la kipaumbele, na kwa namna yeyote, kwa gharama yeyote watalilinda taifa na kulifanya kuwa nchi ya amani.
Katika kufanikisha azma yake kiongozi huyo wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo amesema jitihada za kijeshi, kisiasa na kidiplomasia zinazofanyika sasa zitaendelea katika kutatua tatizo hilo. Rwanda imekuwa ikishutumiwa kwa kuunga mkono uasi nchini humo lakini Kabila hakulitaja taifa hilo katika hotuba yake.
Kiongozi wa waasi katika eneo la machafuko Bosco Ntaganda, mbabe wa kivita anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita kwa tuhuma za uhalifu wa kivita. Jumanne iliyopita ilitoa ripoti iliyosema kuwa afisa wa ngazi ya juu wa ulinzi nchini Rwanda kwa wadhfa wake amekuwa akiwasadia waasi kwa kuwapa silaha na misaada mingine yakiwemo mafunzo.
Majina ya maafisa hao yaliotajwa ni Waziri wa Ulinzi wa Rwanda, James Kabarebe, na Mkuu wa Jeshi la Ulinzi Charles Kayonga. Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Louise Mushikawabo amesema ripoti hiyo inahitaji uchunguzi.
Mwandishi: Sudi Mnette/AFP
Mhariri: Abdu Mtulya