Kabul. Hatima ya mateka 21 wa Korea ya kusini bado haijulikani.
2 Agosti 2007Hatima ya mateka 21 wafanyakazi wa kutoa msaada kutoka Korea ya kusini wanaoshikiliwa na wapiganaji wa Taliban imeendelea kuwa mashakani baada ya muda wa mwisho wa hivi sasa kwa serikali ya Afghanistan kukubaliana na madai ya kundi hilo kumalizika.
Msemaji wa Taliban , hata hivyo amesema kuwa mateka wote 21 bado wahai. Wateka nyara hao wanadai kuwa serikali ya Afghanistan iwaachie wapiganaji wa kundi hilo walioko kifungoni ili kuwaachia mateka hao.
Maafisa wa Afghanistan wameondoa uwezekano wa kubadilishana wafungwa. Wakati huo huo , televisheni ya Al-Jazeera imetangaza video inayomwonyesha mateka wa Kijerumani ambaye alitekwa nyara na wapiganaji wa Taliban nchini Afghanistan. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Ujerumani Julia Groß amesema kuwa kundi la kushughulikia mizozo la wizara yake bado linaendelea kuchunguza video hiyo.
Amesema kuwa wanaelekeza mtazamo wao kwa ujumbe uliomo katika video hiyo kama suala la kutaka kutuogopesha. Wataalamu wa kushughulikia mizozo wanaichunguza kwa makini video hiyo.
Video hiyo inaaminika kuwa imerekodiwa siku kadha zilizopita.