Kagame: Mazungumzo ya usalama wa Rwanda na Burundi yaendelea
21 Desemba 2020Rais Paul Kagame alikuwa akizungumza mubashara kupitia runinga ya taifa akiwa Ikulu mjini Kigali. Waandishi wa habari walikuwa kwenye ukumbi mwingine wa Kigali conference Center ambapo badaye walipewa nafasi ya kuuliza maswali kuhusu masuala mbalimbali.
Pamoja na mambo mengine Rais Paul Kagame amezungumzia usalama katika mpaka hususan juu ya kinachoendelea baina ya Rwanda na mataifa ambayo kwa miaka ya hivi karibuni yamekuwa na matatizo na nchi yake. Amesema kwa sehemu kubwa hali ni shwari, akionya lakini juu ya mapungufu katika baadhi ya maeneo.
"Tatizo kidogo tulilo nalo liko upande wa Kusini kwenye mpaka na majirani zetu, ndugu zetu na jirani zetu wa Burundi, kuna mazungumzo yanayoendelea baina yetu ili kutafuta juhudi za jinsi gani usalama wetu usiendelee kuharibika hasa kuanzia kwa majirani zetu. Upande wa magharibi kunakopatikana nchi ya DRC wao ushirikiano wetu ulianza mapema tangu kulipopatikana mabadiliko ya utawala, naweza kusema kwamba matatizo yaliyokuwepo yanaendelea kupungua kabisa." Amesema Kagame.
Lakini alipokuwa akizungumzia upande wa kaskazini katika mpaka wa Rwanda na Uganda nchi ambayo kimsingi imekuwa na matatizo na Rwanda amesema kuwa hali ijapokuwa haijatengamaa lakini kuna hatua iliyopigwa.
Kuanzia jana jumapili Rwanda ilituma idadi isiyojulikana ya wanajeshi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati siku nne kabla ya nchi hiyo kuingia kwenye uchaguzi mkuu wa Rais. Jeshi la Rwanda lilithibitisha kuondoka kwa kikosi hicho ambacho ilisemekana kinakwenda kuongeza nguvu kwa majeshi ya Rwanda yaliyopo tayari nchini humo ili kulinda usalama wakati wa uchaguzi pamoja na kupambana na wapiganaji wanaongozwa na Rais wa zamani wa nchi hiyo Francois Bozize.
Rais Kagame akasema "Hivi karibuni kulikuwa na mashambulizi ya makundi yaliyotokea mahali fulani kutoka nje ya Jamhuri ya kati lakini likiendeshwa na wana-Jamhuri ya kati, wakaanza kujikusanya pamoja na baadaye nikaambiwa baadhi ya makundi yanamtii Rais wa zamani wa nchi hiyo Francois Bozize, naambiwa lengo lao lilikuwa ni kuharibu uchaguzi mkuu lakini kikubwa zaidi kwetu ni kwamba walishambulia wanajeshi wetu."
Ama kuhusu ugonjwa COVID-19, Rais Kagame amesema Rwanda tayari imeshaweka mikakati mikali kuhusu kupambana na wimbi jipya la maambukizi ya ugonjwa huo ambapo kuanzia siku ya Jumanne tarehe 22 mwezi huu hakuna mtu atakeruhusiwa kutembea baada ya saa mbili za usiku.Rais Kagame amesema kwamba haya yote yanafanyika katika juhudi za kuhakikisha kwamba wanawalinda wananchi dhidi ya janga hili.
"Tumefikia mahali ambapo haaytuwezi kukubali kwamba juhudi zote tulizoziweka kujilinda dhidi ya janga kupotea bure, huu si wakati wa kubweteka isipokuwakuhakikisha mafanikio yetu hayaharibiki." Ni kauli yake Kagame
Zaidi ya watu elfu saba na mia saba ndiyo wamekwishaathirika na ugonjwa Corona nchini Rwanda, huku wengine wapatao elfu sita wakipona na tayari watu 63 wakishapoteza maisha yao.
Mwandishi: Sylivanus Karemera/DW Kigali
Mhariri: Daniel Gakuba