1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kambi ya Tshisekedi yadai ushindi Congo

8 Januari 2019

Timu ya Kampeni ya mgombea urais nchini Congo Felix Tshisekedi, imesema wawakilishi wa kambi yao wamekutakana na kambi ya rais anaemaliza muda wake Joseph Kabila kuhakikisha makabidhiano ya amani ya madaraka.

https://p.dw.com/p/3BCcq
Kongo hält mit zwei Jahren Verspätung historische Wahlen ab
Picha: Reuters/O. Acland

Kambi ya Kabila hata hivyo imekanusha kuwepo na mikutano kama hiyo tangu kufanyika kwa uchaguzi wa Desemba 30, ambao matokeo yake ya awali yanatarajiwa kutangazwa baadae wiki hii.

Uchaguzi huo ulinuwia kuleta mabadiliko ya kwanza ya kidemokrasia nchini Congo katika kipindi cha miaka 59 ya uhuru wake, lakini wasiwasi unazidi kuenea huku baadhi ya wanasiasa wa upinzani wakiituhumu serikali kwa kujaribi kuiba kura.

Matokeo mengine yanayobishaniwa huenda yakazusha aina ya vurugu zilizoshuhudiwa baada ya uchaguzi wa mwaka 2006 na 2011 na kuvuruga tena usalama katika maeneo ya mpakani mwa DRC na Uganda, Rwanda na Burundi, ambako dazeni kadhaa za makundi ya wanamgambo zinaendesha shguhuli zake.

Tshikedi aliwania dhidi ya mgombea alieteuliwa na kabila mwenyewe Emmanuel Ramazani Shadary, na kiongozi mwingine wa upinzani Martin Fayulu, ambaye uchunguzi wa maoni ya wapigakura kabla ya uchaguzi ulimuonyesha akiongoza kinyanganyiro hicho.

DR Kongo Wahlkampf Martin Fayulu
Martin Fayulu akiwa amebebwa na wafuasi wake wakati wa kampeni.Picha: Reuters/S. Mambo

Wasiwasi kwa wafuasi wa Fayulu

Ripoti za mawasiliano kati ya kambi za Tshisekedi na Kabila zimezusha mashaka ya baadhi ya wafuasi wa Fayulu. Wanahofia kwamba huneda Kabila anajaribu kujadili ugawanaji wa madaraka na Tsikesedi ikiwa, kama wanadiplomasia wengi wanavyoamini, Shadary anaburura katika matokeo.

Kwenye mkutano na waandishi habari, katibu mkuu wa chama cha siasa cha Tshisekedi cha UDPS, amesema mawasiliano kati ya kambi mbili yalikuwa yanachangia maridhiano ya kitaifa, na kwamba chama cha UDPS "kinapinga sera yoyote ya kulipiza vizazi".

"Watu hao wawili (Kabila na Tshisekedi) wana maslahi katika kukutana kuandaa mazingira ya amani na ya ustaarabu ya kukabidhiana madaraka," Jean-Marc Kabund alisema. Msemaji wa Tshisekedi, Vidiye Tshimanga, baadae alisema Kabila na Tshisekedi hawajakutana ana kwa ana tangu uchaguzi lakini kwamba wawakilishi wake wamekutana mara kadhaa.

Kabila anatazamiwa kuachia ngazi baadae mwezi huu baada ya kukaa madarakani kwa miaka 18. Kukataa kwake kuondoka wakati muhula wake ulipomalizika rasmi mwaka 2016 kulisababisha maandamano ambamo vikosi vya usalama viliuwa dazeni kadhaa za watu.

Kambi ya Kabila yakanusha kuwepo mawasiliano

Barnabe Kikaya Bin Karubi, moja wa washauri wa Kabila na msemaji wa Shadary, alikanusha kwamba kulikuwepo na mawasiliano yoote na Tshisekedi au wawakilishi wake.

Demokratische Republik Kongo | Emmanuel Ramazani Shadary, Präsidentschaftskandidat in Kinshasa
Mgombea wa muungano wa vyama tawala Emmanuel Ramazani Shadary.Picha: Getty Images/AFP/J. Wessels

Kwenye mkutano wake na waandishi habari siku ya Jumanne, muungano wa vyama tawala umeituhumu kampeni ya Fayulu na Maaskofu wa Congo kwa kujaribu kuchochea vurugu za baada ya uchaguzi katika taifa hilo kubwa lenye utajiri wa madini. Wiki iliyopita, maaskofu hao walisema wanajua mshindi wa uchaguzi, tangazo lililotazamwa na wengi kama onyo kwa mamlaka dhidi ya wizi wa kura.

Kabund alimtaja Tshisekedi kama mshindi wa uchaguzi huo, lakini hakusema alikuwa anajengea hoja yake kwa msingi gani. Kambi ya Shadary ilisema inatarajia kushinda huku kampeni ya Fayulu pia ikisema alikuwa katika nafasi imara ya kuibuka kidedea.

Kasoro kubwa katika kuhesabu kura

Wakati huo huo, ujumbe wa uangalizi wa uchaguzi huo ulisema Jumanne kuwa ulishuhudia kasoro 52 kubwa katika vituo 101 vya kuhesabu kura ulikotuma waangalizi, ikiwa ni pamoja na watu kuchezea matokeo.

Kuna vituo 179 vinavyoendelea kukusanya matokeo nchini Congo kote. Ripoti kutoka shirika la SYMOCEL lenye makao yake nchini Congo imesema asilimia 16 a vituo vya vya kuhesabu kura lilivyoshuhudia vilitegemea matokeo kutoka kwenye mashine badala ya kura zilizohesabiwa kwa mkono kama inavyotakiwa kisheria.

Lilisema asilimia 92 ya vituo vya kuhesabia kura lilivyosimamia havikubandika fomu za matokeo nje kama inavyotakiwa kisheria.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre.

Mhariri: Caro Robi