Kampeni zapigwa marufuku Kinshasa
19 Desemba 2018Huku zikisalia siku tatu za kampeni ya uchaguzi nchini Kongo, Meya wa jiji la Kinshasa amepiga marufuku kampeni ya uchaguzi kwa wagombea wote wa kiti cha urais katika kile anachoelezea kuwa ni sababu za kiusalama.
Wagombea wote walitarajiwa kuitisha mikutano ya hadhara hapa mjini Kinsasa kuanzia leo hadi Ijumaa siku ya mwisho ya kampeni. Kampeni hiyo imegubikwa na visa kadhaa vya umwagikaji wa damu unaotajwa kuhusisha vyombo vya dola na ulipizaji kisasi baina ya wafuasi wa wagombea.
Hatua hiyo ambayo imepokelewa kwa mshangao mkubwa inaelezewa na Andre Kimbuta, meya wa mji wa Kinshasa, kwamba ni katika lengo la kuhakikisha usalama wa mji huu mkuu. Kwenye taarifa yake, Meya Kimbuta amesema kwamba idara za usalama zina taarifa kwamba kumepangwa vurugu nyingi mjini Kinshasa wakati wa mikutano ya hadhara ya wagombea wakuu kwenye uchaguzi wa Jumapili.
Amri hii imetolewa wakati mgombea wa upinzani, Martin Fayulu, akiwa njiani kuelekea Kinshasa akitokea kwenye jimbo jirani la Bandundu, na alitarajiwa kuhutubia wafuasi wake ambao tayari walikusanyika kwenye uwanja Ste Therese mashariki mwa jiji la Kinshasa.
Msemaj wa chama cha Fayaulu amesema kwamba tangazo hilo la meya wa mji linakiuka sheria na wataendelea kumsubiri mgombea wao hadi muda atakapofika. Mashirika ya kutetea haki za binadamu pia yamelalamikia hatua hiyo na kusema ni ukiukwaji wa haki za kujieleza na sheria ya uchaguzi. Georges Kapiamba, kiongozi wa shirika la ACCES a la Justice, amesema hatua hii imechangia katika kuzorota kwa hali ya kampeni hii.
Wagombea wengine ambao walitarajia kuitisha mikutano ya hadhara mjini Kinshasa ni pamoja na Felix Tshisekedi hapo kesho Alhamisi, na mgombea wa chama tawala Emmanuel Ramazani Shadary, Ijumaa - siku ya mwisho ya kampeni.
Lakini meya wa Kinshasa sasa anasema kwamba kampeni hiyo wanaweza kuendesha kupitia vyombo vya habari. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanaelezea kwamba kampeni hii ilikuwa na visa vingi vya kutostahamiliana na umwagikaji wa damu. Georges Kapiamba amesema watu wasiopungua 6 wameuawa toka mwanzo wa kampeni.
Waziri wa mambo ya ndani na mwenziwe wa ulinzi wameelezea kwamba kiwango cha usalama kimezidishwa kote nchini. Na polisi wataungwa mkono na jeshi ikiwa itahitajika kwa ajili ya kulinda usalama wakati wa uchaguzi. Serikali imetangaza pia kwamba siku ya uchaguzi, mipaka ya Kongo itafungwa kwa masaa 24.
Mwandishi: Saleh Mwanamilongo/DW Kinshasa
Mhariri: Mohammed Khelef