1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Angela Merkel ziarani nchini India

Oummilkheir30 Oktoba 2007

Ujerumani yapania kuimarisha ushirikiano wa kisayansi,kiuchumi na kisiasa pamoja na India

https://p.dw.com/p/C7fz
Picha: picture-alliance/ dpa

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amewasili New Delhi kwa ziara rasmi ya siku nne.Mazungumzo ya kansela pamoja na mwenyeji wake,waziri mkuu Manmohan Singh yatatuwama katika masuala ya ushirikiano wa kiuchumi na usalama.

Hii ni ziara ya kwanza ya kansela Angela Merkel nchini India, nchi inayozidi kuangaliwa kama mshirika mkubwa wa kiuchumi kwa Ujerumani.

Biashara ya pande mbili imeongezeka kwa asili mia 40 mwaka jana,na kufikia yuro bilioni 10.

Kansela Angela Merkel aliyefuata na ujumbe wa watu 30 wakiwemo wakuu wa mashirika makubwa makubwa ya Ujerumani,amekua na mazungumzo leo asubuhi pamoja na kiongozi mwenzake wa India,waziri mkuu Manmohan Singh.

“India ni mshirika wetu katika maendeleo ya kisayansi”amesema kansela Angela Merkel na kuishadidia:

“Hii leo nataraji kuchangia katika kuzidi kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya India na Ujerumani,katika sekta ya sayansi,uchumi na siasa.”

Akiandamana na mwenyeji wake waziri mkuu Manmohan Singh,kansela Angela Merkel amebonyeza kifungo kilichopelekea kuondoka treni ya kiufundi iliyopewa jina “Science Express”,yenye mabehewa 13.Mashirika kadhaa ya Ujerumani ikiwa ni pamoja na BASF na Bosch yamechangia katika kutengeneza treni hiyo ya ufundi wa hali ya juu.

Treni hiyo inayoonyesha ufundi wa hali ya juu wa Ujerumani,itazunguka katika miji 56 ya India katika kipindi cha miezi ijayo.

“Tunataka kuwavutia zaidi vijana wakubali kujipatia mafunzo katika sekta ya kisayansi nchini India na Ujerumani” amesema kansela Angela Merkel.

“Treni hii itaeneza maajabu ya kisayansi mpaka katika maeneo ya mbali kabuisa ya nchi yetu” ameshadidia kwa upande wake waziri mkuu Manmohan Singh.

Kansela Angela Merkel amepangiwa pia kuzungumza na rais PRATIBHA PATIL,waziri wa mambo ya nchi za nje PRANAB MKHERJEE na mwenyekiti wa chama tawala cha Congress bibi Sonja Gandhi.Mazungumzo ya kina pamoja na waziri mkuu Manmohan yatafanyika leo jioni.

Makubaliano yanatazamiwa kutiwa saini katika sekta ya ushirikiano wa kisayansi na kijeshi pamoja pia na haki miliki.Kansela Angela Merkel atajaribu kuwatanabahisha wenyeji wake umuhimu wa kujiunga na juhudi za kupunguza hali ya ujoto ulimwenguni.

Kesho kansela Angela Merkel atautembelea mji mkuu wa kiuchumi Mumbai au Bombay kama mji huo ulivyokua ukijulikana hadi mwaka 1995.