1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel awasili India lakini amechelewa

31 Mei 2011

Kansela Angela Merkel awasili New Delhi

https://p.dw.com/p/11RBT
Kansela Angela Merkel wa UjerumaniPicha: AP

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, akichelewa kwa masaa mawili, amewasili katika mji mkuu wa India, New Delhi, kwa mashauriano ya kwanza baina ya mawaziri wa Ujerumani na wenziwao wa India. Sababu ya Kansela kuchelewa kuwasili New Delhi ni kwamba kwa muda mfupi Iran ilikataa ndege aliosafiria Bibi Merkel kuruka juu ya anga ya nchi hiyo. Sababu ya kuchukuliwa hatua hiyo haijulikani. Ndege ya pili iliokuwa na mawaziri wa nne wa Ujerumani ndani yake iliweza kuruka juu ya anga ya Iran bila ya matatizo yeyote.

Mwenyewe Kansela Merkel alisema hajawahi kushuhudia mkasa kama huo; pia marubani waliokuwa wakiiendesha ndege hiyo. Ndege hiyo, aliokuwa akisafiria Kansela, ikiwa pia na ujumbe mkubwa ndani yake, ilibidi jana usiku ibadilishe njia na izunguku kwa masaa mawili juu ya anga ya Uturuki, kabla ya kupata kibali cha kuvuka juu ya anga ya Iran. Sababu hazijulikani.

Kwa mujibu wa serikali ya Ujerumani ni kwamba kabla ya kuondoka ndege hiyo kutoka Berlin, ruhusa ilitolewa kwa ndege hiyo kuruka juu ya anga ya Iran. Lakini upande wa Iran unabisha jambo hilo. Ndege ya pili ya serikali ya Ujerumani, ambapo ndani yake walikuwemo mawaziri na manaibu wa mawaziri wa Ujerumani waliokuwa wanakwenda katika mashauriano ya kwanza baina yao na wenziwao wa India, iliweza kupita juu ya anga ya Iran bila ya matatizo .

Merkel Westerwelle Deutschland Kabinett
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, na Kansela Angela MerkelPicha: AP

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, alitoa tamko kuhusu mkasa huo:

"Kuzuiliwa kwa safari ya Kansela wa Ujerumani ni jambo lisilokubalika kabisa, ni kutoonesha heshima kuelekea Ujerumani, jambo ambalo hatulikubali. Nimemwita balozi wa Iran mjini Berlin, na tutaweka wazi kabisa kwamba kwenda kinyume namna hivyo dhidi ya safari za kimataifa za ndege kutoka Ujerumani hakutakubaliwa kwa namna yeyote ile."

Kiini cha mawashauriano ya Kansela Merkel na mawaziri wake pamoja na wafanya biashara wa Kijerumani huko India ni kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi na wa teknolojia na nchi hiyo ya Asia; na masuala watakayoyapa kipa umbele katika mazungumzo yao ni elimu, usafiri na nishati. Zaidi ya hayo, kuna suala la kuuziwa India ndege za kivita 126 aina ya Eurofighter. Ujerumani inapigania mkusanyiko wa makampuniy a Ulaya yanayoitengeneza ndege hiyo ipate biashara hiyo yenye thamani ya Rupia za India bilioni 12.

Inafikiriwa pia masuala mawili yanayozigawa nchi hizi mbili-Ujerumani na India- yatagusiwa katika mazungumzo ya Bibi Merkel na waziri mkuu wa India, Manmohan Singh, nayo ni kuteuliwa kwa mkuu mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, na matumizi ya nishati ya kinyukliya. Ujerumani imemuunga mkono mtetezi wa nchi za Umoja wa Ulaya, Bibi Christine Lagard, kwa wadhifa wa kuwa mkuu wa IMF, huku kukiweko mgawanyiko kati ya nchi zilizoendelea na zile zinazoendelea juu ya uendeshaji wa shirika hilo la kimataifa linalotoa mikopo. Kwa desturi, shirika la IMF limekuwa likiongozwa na mtu kutoka nchi ya Ulaya, huku Benki ya Dunia ikiongozwa na Mmarekani. Lakini nchi zinazoendelea zinazidi kuupinga utaratibu huo.

Nayo India pia imetangaza mipango ya kuengeza sana uwezo wake wa kutoa nishati ya kinyukliya na imekuwa ikifanya mazungumnzo na Russia, Ufaransa, Japan na makampuni ya Kimarekani ili kujenga vinu vipya vya kinyukliya nchini humo. Hivi sasa asilimia tatu ya nishati ya India inatokana na nguvu ya kinyukliya, wakuuwa New Delhi wanataka kuengeza ifikie asilimia sita mwishoni mwa mwongo huu na asilimia 13 ifikapo mwaka 2030.

Ujerumani ni mshirika mkubwa wa kibiashara wa India kutoka Ulaya; biashara kati ya nchi hizo mbili ikifikia Euro bilioni 15.4 mwaka 2010, ikitarajiwa itaongezeka hadi kufikia Euro bilioni 20 mwaka 2012.

Mwandishi: Othman Miraji

Mhariri: Josephat Charo