1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KENENISA BEKELE 'MWANARIADHA WA MWAKA' DUNIANI

20 Septemba 2004
https://p.dw.com/p/CEHZ

MICHEZO

-LIGI MASHUHURI BARANI ULAYA

-MWANARIADHA WA ETHIOPIA KENENISA BEKELE NA YELENA ISINBAYEVA WA RUSSIA WATEULIWA ‘WANARIADHA WA MWAKA’

Tuanze na Ligi mashuhuri barani Ulaya mwishoni mwa wiki hii:

Katika Bundesliga-Ligi ya ujerumani, Wolfsburg iliparamia kilele cha Ligi hapo jumamosi kufuatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Hansa Rostock wakati Stuttgart ilimudu suluhu tu 0:0 na Hertha Berlin.Sare ya Berlin ni ya 5 mfululizo.

Mabingwa mara kadhaa-Bayern munich walitoka nyuma baada ya kuizabwa mabao 2:0 na mwishoe kusawazisha 2:2 kati yake na Borussia Dortmund.

Kufuatia changamoto 5 za kwanza za msimu huu, Wolfsburg kwa mara ya kwanza wanaongoza orodha ya Ligi kwa pointi 12 ,wakifuatwa nyuma nafasi ya pili na Stuttgart yenye pointi 11.Mabinghwa Bremen wanafuata nafasi ya tatu kwa pointi 9 kufuatia ushindi wao wa mabao 3:0 dhidi ya jirani zao Hannover 96.

Klabu 3 za miji mikuu-Real madrid ya Spain;AS roma ya Itali na Paris St.Germain, zote zimeshindwa kufua dafu mwishoni mwa wiki na hivyo kuzitia hatarini kazi za makocha wao.

Real Madrid iliozabwa mabao 3-0 katika Champions League kati ya wiki iliopita katika mpambano wake na Bayer Leverkusen ya Ujerumani,ilizabwa bao 1:0 na Espanyol licha ya kuwaacha nje akina David Beckham na raul.Mambo yalipozidi unga, kocha Camacho ametishia kujiuzulu, wengine wanadai ameshajiuzulu.

Nchini Itali, stadi wa Ufaransa David Trezeguet alipiga hodi langoni mara mbili na kuitikiwa katika ushindi wa mabao 2:0 wa klahu yake ya Juventus dhidi ya Atalanta. AS Roma imezabwa mabao 4-3 na Messina licha ya mabao 3-hattrick aliotia stadi wao Vicenzo Montella.

Na nchini Uingereza mabingwa Arsenal walipoteza pointi zao za kwanza msimu huu walipotoka sare 2:2 na Bolton Wonderers huko Highbury.Hatahivyo, Arsenal inaongoza Ligi ya uingereza kwa pointi 2.

Katika Ligi ya Ufaransa, Toulose imepoteza nafasi ya usoni ya ngazi ya Ligi baada ya kukumtwa bao 1:0 na Olympique Marseille.

MICHEZO YA OLIMPIK YA WALEMAVU:

Katika michezo ya olimpik ya walemavu mjini Athens, ugiriki iliofunguliwa Septemba 17,wanariadha 2 walemavu wa Afrika kusini ambao kuumia kwao katika mchezo wa rugby kuliwanyima fursa za kutia fora katika mchezo huo,wametia fora katika michezo hii ya walemavu:

Fanie Lombaard,alienyakua medali 3 za dhahabu katika michezo ya Olimpik ya sydney,2000 ameshinda medali zaidi za dhahabu .Mara hii ametwa ushindi katika kurusha gololi la chuma-short put kwa masafa ya rekodi ya dunia ya mita 13.81.Nae Troye Colins, muafrika Kusini anaeshi wakati huu mjini London,alitia pointi 13 katika ushindi wa mchezo wa rugby wa mabao 27-22 dhidi ya Ubelgiji.

RIADHA:

Katika mashindano ya mwisho ya riadha ya kimataifa msimu huu mjini Monaco,Ufaransa,muethiopia Kenenisa Bekele ameteuliwa ‘mwanariadha bora wa mwaka’ upande wa wanaume wakati ule wa wanawake, taji limeenda kwa mrusi Yelena Isinbayeva ,bingwa wa olimpik katika kuruka kwa upongoo-pole vault.

Wanariadha hawa wawili wamewarithi kitini akina Hicham El gerouj wa Morocco na Hestrie Cloete-mrukaji High-jump wa Afrika Kusini.

Kabla ya mashindano haya ya Monaco, Bekele aliweka rekodi 2 za dunia mnamo muida wa siku 8.

Mei 31 mwaka huu akikimbia huko Hengelo,Uholanzi,Bekele aliivunja rekodi ya Gebre-selassie ya masafa ya mita 5000 kwa muda wa dakika 12,37.35.halafu Juni 8, akikimbia mjini Osttrava,Jamhuri ya Czech,aliivunja rekodi nyengine ya Bekele ya mita 10.000 kwa muda wa dakika 26, 20.31.Isitoshe, Kenenisa Bekele ameshinda mwaka huu kwa mara ya tatu mfululizo mbio za nyika ulimwenguni-world cross-country championship.

Katika changamoto ya mita 3000 kuruka viunzi mjini Monaco,mzaliwa wa Kenya naekimbia chini ya bendera ya Qatar, Saeed Saif Shaheen,zamani akiitwa Stephen Cherono,ameshinda masafa hayo akiwapiku wakenya wote 3 waliotwaa medali za olimpik mjini Athens. Saeed Saif Shaheen ndie bingwa wa rekodi ya dunia wa masafa ya mita 3000 kuruka viunzi na bingwa wa dunia halkadhalika.wakenya walimzuwia kukimbia katika michezo ya Olimpik ya Athens.