Kenya: IEBC yasema matayarisho yote ya uchaguzi yamekamilika
8 Agosti 2022IEBC iliyaeleza hayo mapema leo Jumatatu kwenye ukumbi wa Bomas of Kenya walipokuwa wakielezea mfumo mzima wa kupiga kura. Vituo vyote 46,000 zitafunguliwa alfajiri ili wakenya milioni 22.1 wapige kura kutwa nzima hadi jioni.
Soma zaidi: Wagombea wa uchaguzi Kenya na kampeni za mwisho
Imearifiwa kuwa mchakato huo utamchukua mpiga kura dakika tatu kuitimiza haki yake endapo hahitaji usaidizi wa aina yoyote. Kila mpiga kura atapewa karatasi sita za rangi tofauti kuwachagua rais, gavana, seneta, mwakilishi wa wanawake, mbunge na mwakilishi wa wadi.
Vifaa vyote muhimu vimefikishwa vituoni
Mashine 55,000 za kielektroniki za kuwatambua wapiga kura zitatumika. Kila wadi itapewa mashini 6 za ziada kutumika endapo hitilafu yoyote inatokea. Ijapokuwa mfumo wa kuwatambua wapiga kura ni wa dijitali, daftari asilia litatumika pia kama ilivyoamuru mahakama kuu hasa katika maeneo yasiyokuwa na huduma za mtandao wa 3G.
Wafungwa pia wataweza kupiga kura ila kumchagua rais pekee. Jumla ya wafungwa 10,000 wamesajiliwa kupiga kura mwaka huu. Kwa atakayeharibu karatasi za kupigia kura, maafisa wa tume ya uchaguzi watakuwa vituoni kutoa usaidizi.
Soma zaidi: Raila: Sishiriki mdahalo sababu Ruto ni fisadi
Kwa mujibu wa tume ya IEBC, waangalizi 10,000 wanashiriki kwenye mchakato wa uchaguzi huu. Asilimia kumi (10%) ya waangalizi hao wanatokea mataifa ya kigeni na wengine ni Wakenya. Ujumbe wa IGAD ulizinduliwa siku ya Jumapili baada ya kuhitimisha mafunzo. Rais wa zamani wa Ethiopia Mulatu Teshome ndiye anayeuongoza ujumbe huo.
IGAD ina wajumbe 24 wanaotokea mataifa 6 wanachama na watakuwa kwenye kaunti 10.Matokeo kamili yanatarajiwa kutangazwa kabla tarehe 16.
Maafisa wa uchaguzi watimuliwa
Katika taarifa nyingine, IEBC imewafuta kazi maafisa wake wanne ambao waligundulika kufanya mkutano wa faragha nyumbani kwa mgombea wa nafasi ya uwakilishi wa bunge la kaunti huko Homa Bay. Tume hiyo imesema maafisa hao wamekiuka sheria kutokana na maafisa kutotakiwa kuegemea upande wa kisiasa.
Soma zaidi: Matiangi: Tumejiandaa kuilinda Kenya wakati wa uchaguzi
Aidha, Mamlaka inayosimamia utendaji kazi wa maafisa wa polisi nchini Kenya, IPOA, itafuatilia mienendo ya maafisa wa polisi kote nchini humo wakati huu wa uchaguzi. Kwenye chaguzi zilizopita polisi wamelaumiwa kuwanyanyasa na kukiuka haki za watu, hasa kunapotokea vurugu ama maandamano kuhusu uchaguzi.