1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya na Tanzania hazitacheza dimba la AFCON

4 Agosti 2014

Kenya na Tanzania zimebanduliwa nje ya kempeni ya kufuzu katika dimba la Kombe la Mataifa ya Afrika - AFCON litakaloandaliwa hapo mwakani nchini Morocco.

https://p.dw.com/p/1CoiB
Tresor Mputu Fußballspieler Kongo
Picha: Getty Images

Lakini hakikuwa kilio na ghadhabu katika eneo hilo la Afrika Mashariki, kwa sababu Uganda iliizaba Mauritania na kufuzu katika awamu ya makundi, ambayo inaanza mwezi Septemba.

Harambee Stars ya Kenya ilimudu tu sare ya sifuri kwa sifuri dhidi ya “Mamba” wa Lesotho mjini Nairobi, licha ya kuutawala mchezo na hivyo kuondolewa kwa jumla ya goli moja kwa sifuri kutokana na ushindi wa Lesotho katika mkondo wa kwanza. hatua hiyo ililifanya Shirikisho la Soka Kenya FKF kukitimua kikosi kizima cha kiufundi cha timu ya taifa kikiongozwa na kocha Adel Amrouche. Mmoja wa wachezaji gwiji wa soka Kenya Joe Kadenge ni miongoni mwa wakenya walioshutumu matokeo hayo mabaya nchini Kenya.

Joe Kadenge Fußballlegende aus Kenia
Mchezaji nguli wa soka Kenya Joe Kadenge asema Kenya inahitaji kufanya mageuzi makubwa katika mchezo wa kandandaPicha: DW/R. Kyama

Msumbiji iliizika Tanzania kwa kuwafunga magoli mawili kwa moja katika uwanja wa Zimpeto mjini Maputo. Hivyo walifuzu kwa jumla ya magoli manne kwa matatu baada ya timu hizo mbili kutoka sare ya magoli mawili kwa mawili katika mechi ya kwanza.

Msumbiji wameingia katika Kundi F, ambapo watapambana na mabingwa wa Afrika mwaka wa 2012 Zambia, Visiwa vya Cape Verde na Niger.

Uganda ambayo iliishinda Mauritania magoli mawili kwa sifuri dhidi ya Mauritania, ilipata ushindi wa goli moja kwa sifuri ugenini katika uwanja wa Olympique mjini Nouakchott.

Uganda sasa wanaingia katika Kundi E ambapo watamenyana na Ghana, Togo na Guinea. Rwanda pia ilijizatiti dhidi ya mpinzani mkubwa kwa kuizaba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo magoli mawili kwa bila na kuupeleka mchuano huo katika awamu ya matuta. Rwanda ilishinda kwa magoli manne kwa matatu huku kipa wa Rwanda Jean Luc Ndayishimiye akiwa shujaa kwa kuokoa penalty tatu.

Malawi pia ilijikatia tikiti ya makundi kupitia mikwaju ya penalty dhidi ya Benin. Botswana iliichabanga Guinea Bissau magoli matatu kwa moja.

Sierra Leone ilifuzu bila ya kucheza mchuano wa mkondo wa pili dhidi ya USHELISHELI wakati nchi hiyo ilipoamua kususia mchuano huo badala ya kuwaruhusu wachezaji wa Sierra Leone kusafiri kwa sababu ya hofu ya kusambaa virusi vya ugonjwa hatari wa Ebola.

Kundi A: Nigeria, Afrika Kusini, Sudan, Rwanda
Kundi B: Mali, Algeria, Ethiopia, Malawi
Kundi C: Burkina Faso, Angola, Gabon, Lesotho
Kundi D: Ivory Coast, Cameroon, DR Congo, Sierra Leone
Kundi G: Tunisia, Misri, Senegal, Botswana

Mechi za makundi za kufuzu katika dimba la CAN 2015 zitaanza mwezi Septemba hadi Novemba.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Rueters/APE
Mhariri: Mohammed Khelef