Kenya yakabiliwa na uhaba wa gesi ya oksijeni
8 Aprili 2021Hospitali za kaunti zinalazimika kuahirisha shughuli za upasuaji usiokuwa wa dharura ili kuweza kupambana na uhaba huo.
Uhaba wa gesi ya oksijeni hospitalini umelikumba taifa wakati ambapo idadi ya wagonjwa mahututi na walioambukizwa covid 19 inaongezeka.
Soma pia: Janga la COVID-19 lazidisha ukiukwaji wa haki za binadamu
Hospitali kuu ya Kenyatta imejikuta pabaya kwani inapokea wagonjwa wengi ukizingatia kuwa ni ya rufaa na kitaifa.Matumizi ya gesi hiyo yameongezeka maradufu tangu mwaka uliopita.Ili kujaribu kukidhi mahitaji ya wagonjwa mahututi, shughuli za upasuaji usiokuwa wa dharura zimeahirishwa.
Takwimu za baraza la magavana zinaashiria kuwa kwa jumla vipo viwanda 58 vya kutengeza gesi ya oksijeni kwenye kaunti zote 47 ila ni 42 vinavyofanya kazi kwa sasa.Mwenyekiti wa kamati ya afya ya baraza la magavana Profesa Anyang Nyongo aliyepia gavana wa kaunti ya Kisumu anafafanua kuwa mitungi 2828 ya gesi ya oksijeni na vifaa vyengine vipo pamoja na vitanda 3601 vya wagonjwa mahututi vilivyounganishwa na mifereji ya gesi ya oksijeni kote nchini.
Amnesty International yaeleza madhila yaliyosababishwa na COVID-19
Kwa mujibu wa wizara ya afya,Kenya ilitengeza na kuhitaji tani 410 za gesi ya oksijeni mwaka uliopita.Hata hivyo kwa sasa kwa sababu ya janga la corona, idadi ya wagonjwa mahututi imeongezeka na mahitaji ya gesi hospitalini yameongezeka maradufu.Kadhalika inasadikika kuwa mitungi 20,000 ya gesi ya oksijeni imetelekezwa kote nchini na kila mmoja unauzwa kwa shilingi alfu 40.
Wiki iliyopita kampuni ya Devki ya uhandisi na vyuma ilijitolea pasina malipo kugawa gesi ya oksijeni kwa hospitali kadhaa. Narendra Raval ni mwenyekiti wa kampuni ya Devki iliyo na viwanda vya kutengeza gesi ya oksijeni katika miji ya Mombasa, Ruiru na Athi River.
Kwa upande wake Waziri wa Afya wa Kenya Mutahi Kagwe anawarai wanaohodhi mitungi ya gesi ya oksijeni kuiachilia ili kuziba pengo lililoko la uhaba.Wizara hiyo hiyo iko kwenye harakati za kufikia mwafaka na ile ya Fedha kusaka suluhu na uwezekano wa kupunguza kodi inayotozwa mitungi ya gesi ya oksijeni.