Kenya yaomboleza kifo cha Prof. Saitoti
11 Juni 2012Hisia mbali mbali zinaendelea kutolewa miongoni mwa Wakenya kufuatia ajali ya helkopta ya hapo jana iliyosababisha vifo vya Waziri wa Usalama wa Kitaifa, Prof. George Saitoti, Naibu wake, Orwa Ojode, walinzi wao wawili na marubani wawili wa ndege hiyo. Wengi wamepigwa na butwaa kufutaia habari za mkasa huo ambao hadi sasa kiini chake haijabainika.
Baadhi ya viongozi wamewataja Saitoti na Ojode kuwa maafisa waliojitolea kuihudumia serikali. Waziri Mkuu Raila Odinga amesema uchunguzi umeanzishwa kubainisha chanzo cha ajali hiyo.
“Ni mkasa mkubwa kwa taifa la Kenya uchunguzi unaendelea na tutasema mengi baadaye”
Kauli kama hiyo imetolewa na waziri wa Turati za Kitaifa William Ole Ntimama, huku Naibu Waziri Mkuu, Musalia Mudavadi, akimtaja Ojode kama mbunge aliyejitolea kwa ukakamavu kuitetea serikali bungeni.
Ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa tatu asubuhi wakati Waziri Saitoti na Naibu wake walipokuwa wakielekea kaskazini mwa nchi kwa mkutano wa kuchangisha pesa katika Kanisa moja nyumbani kwa Orwa Ojode.
Kufuatia msiba huo, Rais Mwai Kibaki ametangaza siku tatu za kuomboleza huku bendera zikipeperushwa nusu mlingoti na wakati huo huo kuitisha mkutano wa dharura wa baraza la mawaziri ambao unaendelea wakati huu katika jumba la mikutano ya kimataifa KICC hapa Nairobi.
Rais Mwai Kibaki anatarajiwa kutoa hotuba kwa taifa baadaye leo (12 Juni 2012) saa 10:00 alasiri.
Ripoti: Alfred Kiti/DW Nairobi
Mhariri. Saumu Yusuf