Marufuku kusafiri miji iliyoathirika na corona Kenya
6 Aprili 2020Akilihutubia taifa leo alasiri, Rais Uhuru Kenyatta alibainisha kuwa madhumuni ya marufuku hiyo ya usafiri ni kuupunguza uwezekano wa virusi vya corona kusambaa.
Usafiri kutoka nje na kuingia ndani ya kaunti ya Nairobi unasitishwa kuanzia usiku wa leo na katika kaunti za Mombasa, Kwale na Kilifi katika ukanda wa pwani ni kuanzia Jumatano wiki hii. Rais Kenyatta amesisitiza pia kuwa hakuna usafiri wowote utakaoruhusiwa hata kwa bodaboda na baiskeli wakati wa usiku katika kaunti za Nairobi, Mombasa, Kilifi na Kwale.
Hata hivyo magari ya kusafirishia vyakula yanaruhusiwa kuendelea na shughuli zao ila kwa masharti ya kuwa na dereva na wasaidizi wasiozidi wawili pekee.
Kadhalika wakazi wa mitaa ya mabanda watapata afueni kwani serikali imeamuru wapate maji pasina malipo ili waweze kuosha mikono kila inapohitajika. Jee wakazi wa mitaa ya mabanda wamepokea vipi taarifa hizo? Baadhi niliokutana nao mtaani Ngomongo walikuwa na haya ya kusema.
Ni lazima kwa kila mkenya kuvalia barakoa kujinga na virusi vya Corona
Kwa sasa kila mkenya analazimika kuvaa barakoa anapoelekea nje kwenye sehemu za umma kama sokoni na kwenye maduka ya jumla.
Kwa upande wake wizara ya afya imeamuru kila anayefariki kwa sababu ya ugonjwa wa COVID 19 azikwe katika kipindi cha saa 24 na jamaa wasiozidi 15 pekee ndio watakaohudhuria maziko. Waziri wa afya Mutahi Kagwe anasisitiza kuwa waliowekwa kwenye karantini watasalia huko kwa siku 14 za ziada ili kuwa na uhakika.
Tangazo hilo limezua hisia mseto kutoka kwa familia na jamaa za walioko kwenye karantini hasa katika taasisi za serikali kwa kuhofia maambukizi baada ya vipimo vya mwanzo. Kadhalika usafiri wa ndege za kimataifa umesitishwa kwa mwezi mmoja zaidi kuanzia leo. Kufikia sasa jumla ya watu 4277 wamepimwa kubaini iwapo wameambukizwa COVID 19.
Yote hayo yakiendelea, shehena ya pili ya msaada wa vifaa vya kupambana na homa hiyo uliotolewa na mfanyabiashara mkubwa wa China Jack Ma inatarajiwa kuwasili wakati wowote kutoka sasa. Mchango huo utasambazwa kwa mataifa 54 barani Afrika na shehena iko njiani.
Thelma Mwadzaya, DW Nairobi