1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi inayomkabili Malema yaahirishwa tena

3 Agosti 2015

Kiongozi wa chama cha Wapigania Uhuru wa Kiuchumi cha Afrika ya Kusini, Julius Malema, amepandishwa kizimbani leo (03.08.2015) kukabiliana na mashitaka ya rushwa, utakatishaji fedha haramu na uwongo.

https://p.dw.com/p/1G8uK
Julius Malema
Julius Malema katika mahakama ya Polokwane Jumatano 26.09.2012Picha: dapd/AP Photo/Themba Hadebe

Kesi ya Malema imeahirishwa tena miaka mitatu tangu aliposhitakiwa mara ya kwanza. Kesi hiyo imecheleweshwa leo kutokana na mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo kutofika mahakamani baada ya kulazwa hospitalini wiki iliyopita. Mawakili wa Malema wanataka ashitakiwe peke yake, huku serikali ikishinikiza kesi hiyo iahirishwe hadi mapema mwaka 2016. Uamuzi unatarajiwa kutolewa na mahakama kuu ya Polokwane kesho Jumanne.

Ni kijana, ni mtu wa kupiga kelele kutetea haki, haogopi, ana msimamo mkali na amepandishwa kizimbani. Julius Malema, mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Wapigania Uhuru wa Kiuchumi - Economic Freedom Fighters, EFF, nchini Afrika Kusini. Anapendwa sana na wapigaji kura vijana - kama mkosoaji mkubwa wa serikali.

Julius Malema hatafuni maneno, hana kigugumizi. "Wafanyakazi wa nyumbani, walinzi, wachimba migodi - aibu kwenu kwa kukichagua chama cha ANC". Malema anajulikana kwa mashambulizi ya aina hii dhidi ya serikali ya Afrika. Aliwahi kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana katika chama cha African National Congress, ANC. Leo hii kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 34 anashikilia nafasi ya juu ya chama kipya chenye msimamo mkali, ambacho kimezigusa hisia za wengi. Malema na chama chake tayari amefanya sherehe kubwa mbele ya maelfu ya watu katika uwanja wa mpira wa Rustenburg.

Miaka miwili iliyopita wakati Malema alipokiasisi chama hicho, mambo yalikuwa tofauti. Hakuna aliyedhani kingefaulu, amesema mchambuzi wa msuala ya siasa Desai Ashwin kutoka chuo kikuu cha Johannesburg wakati wa mahojiano na DW. "Licha ya ukosoaji wote chama cha EFF kimeimarika na kuwa na nguvu." Wakati wa uchaguzi wa mwaka 2014 kilijishindia viti 25 vya ubunge.

Hilo halikuwa jambo la kawaida kwa Afrika Kusini kwa sababu makundi mengine madogo yaliyojitoa kutoka kwa chama tawala cha ANC hayakuwahi kufaulu namna hiyo, ameeleza Ashwin. Na pamoja na hayo: "Chama cha EFF kimekua na kuwa chama cha upinzani chenye nguvu kinachopendwa na chenye ushawishi mkubwa kinachokipa changamoto kubwa chama cha ANC bungeni kila wakati fursa inapojitokeza."

Südafrika Präsident Jacob Zuma
Rais Zuma alipolihutubia taifa Cape Town (12.02.2015)Picha: AFP/Getty Images/R. Bosch

Hata hivyo Malema analazimika kujibu madai mazito dhidi yake. Leo amepandishwa kizimbani katika mahakama kuu ya Polokwane. Mashitaka ni: Rushwa, udanganyifu na ulanguzi wa fedha. Tayari mwaka 2009, alipokuwa kiongozi wa vijana wa ANC, inadaiwa alihusika na utoaji kandarasi ya serikali ya thamani ya randi milioni 4.1(takriban euro 300,000) kwa kampuni ya ujenzi ya On-Point. Yeye alimiliki hisa katika mapuni hiyo. Kesi hiyo ilitakiwa kuanza kusikilizwa mwaka 2013 lakini ikaahirishwa mara kadhaa. Mbali na Malema kuna viongozi wawili wa kampuni ya On-Point, Lesiba Gwangwa na Kagisho Dichabe, waliofikishwa mbele ya mahakama.

Kutoka Mfuasi hadi Mkosoaji mkali

Rais wa Afrika Kusini Jacbo Zuma aliruhusu mfuasi wake wa zamani afukuzwe kutoka chama cha ANC mwaka 2012. Tangia hapo Malema amekuwa mkosoaji mkali, akimshutumu Zuma na chama tawala hususan kwa rushwa. Mwanasiasa huyo kijana mwenyewe anatakiwa kujibu mashitaka mbele ya mahakama kwa kukwepa kulipa kodi mara kwa mara na kufanya udanganyifu. "Ukilinganisha madai ya rushwa dhidi ya rais Zuma na chama chake, Malema ni samaki mdogo," amesema mchambuzi wa siasa Ashwin. Zuma anashutumiwa kwa matumizi mabaya ya fedha za umma wakati wa ujenzi wa makazi yake kutumia mamilioni ya fedha za walipakodi.

Kwa mujibu wa Ashwin ukosoaji wa Malema haujatiliwa maanani Afrika Kusini. Imekuwa ni kama kumpigia mbuzi gitaa. "Vijana hawakisikilizi tena kwa shauku kubwa chama fisada kinachotawala, ambacho kwa muda mrefu kilisifika kwa kuukomesha ubaguzi wa rangi mwaka 1994."

Maneno matamu ya uongo

Mchambuzi wa masuala ya siasa wa Afrika Kusini Ralph Mathekga hajashawishika kwamba chama cha EFF kinaweza kuubadili mfumo uliopo sasa. "Kikiwa na asilimia chini ya saba ya viti bungeni ushawishi wake si mkubwa hivyo kuweza kukishinikiza chama tawala."

Fauka ya hayo Malema anapendwa. Yeye na chama chake huzungumza kwa niaba ya raia wa kawaida wa Afrika Kusini na tabaka la wafanyakazi, ambao maoni yao yanapuuzwa na rais Zuma. Malema, ambaye mwenyewe ni mwana wa kiume wa mfanyakazi wa nyumbani kutoka mkoa wa Limpopo, ameitisha kutaifishwa kwa migodi ya Afrika Kusini na ugawaji upya wa mashamba makubwa ya wazungu.

Wahlkampf aus Südafrika von Julius Malema 04.05.2014
Julius Malema wakati wa mkutano wa mwisho wa kampeni (04.05.2014)Picha: picture-alliance/dpa

Ralph Mthekga anaona wito huo una uhalali mdogo. "Hiyo ni kaulimbiu tu ya uchaguzi. Ingawa chama cha EFF kinadai kinawapigania masikini, viongozi wake wanapeleka magari ya kifahari ya gharama kubwa - BMW, Mercedes au Range Rover." Pamoja na hayo inakuja kashfa ya ukwepaji kodi ya Malema. Hiyo inaonesha vipi Malema ana heshima ndogo sana kwa wananchi. Kama kweli anawatetea watu wa kawaida, kwa nini halipi kodi yake? Hiyo ingewanufaisha sana masikini," amekosoa Mthekga. Kwa mwenendo wake wa kujitakia makuu Malema hajajitofautisha na wanasiasa wengine wa Afrika Kusini.

Kurejea tena katika ulingo wa siasa

Malema anapenda kukosolewa: Amezowea: Mwaka 2010 na 2011 alishitakiwa kwa uchochoezi wa kisiasa alipouimba wimbo "Kill the Boer" - "Muue Mboer", ambao umepigwa marufuku nchini Afrika Kusini. "Malema anavutia kwa sababu kila mara aliinuka tena," amesema mtalamu wa siasa Ashwin. Watu walidhani Malema amekwisha kisiasa wakati alipofukuzwa katika Umoja wa Vijana wa ANC, lakini wakamuamini tena alipoasisi chama cha EFF na hatimaye kurejea bungeni. Kila mara alifaulu kuishinda mitihani iliyomkabili katika ulingo wa siasa uliotawaliwa na chama cha ANC.

Lakini je Malema ni kiongozi kwa ajili ya Afrika Kusini? Desai Ashwin ana shaka. Jambo moja liko wazi, anasema: "Tangu chama cha EFF kilipoingia bungeni, siasa za Afrika Kusini zimekuwa za kusisimua zaidi."

Mwandishi: Krinninger, Theresa (HA Afrika)

Tafsiri: Josephat Charo

Mhariri: Mohammed Khelef