Salva Kiir agoma kusaini makubaliano ya amani
18 Agosti 2015Upande wa uasi unaoongozwa na Riek Machar ulisaini mkataba huo wa amani, ila rais Kiir na serikali yake hawakufanya hivyo, na mpatanishi alisema kuwa bado serikali ina wasiwasi na masuala kadhaa na itarejea tena katika mazungumzo ya amani ndani ya siku 15 baada mashauriano baina yao.
"Tulitegemea rais Kiir angesaini mpango huo wa utekelezaji. Sijajua kama ameamua kutousaini. Kwa sababu nilipoingia ndani ya chumba cha mazungumzo, nilikutana naye hapa, tukasalimiana, lakini dakika kumi baadaye, niliambiwa kuwa amekataa kusaini. Nilishindwa kumuelewa, hakuwa na sababu yoyote ya kufanya hivyo," alisema Mkuu wa uasi Riek Machar, akiwa katika mkutano huwo huku akionyesha kushangazwa na uamuzi wa Salva Kiir.
Marekani tatishia shinikizo
Halikadhalika msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani John Kirby amesema, Marekani imesikitishwa sana kuwa serikali ya Sudan Kusini iliamua kutosaini mkataba huo ambao unaungwa mkono na Jumuiya ya ushirikiano ya nchi za mashariki mwa Afrika na pembe ya Afrika IGAD, kundi linalojumuisha nchi tatu - Marekani, Uingereza, na Norway - pamoja na China, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.
Kirby ameongeza kuwa Marekani inaitolea wito serikali ya Sudan Kusini kusaini makubaliano hayo ya amani, ndani ya siku kumi na tano walizoziomba kwa kufanya mashauriano baina yao. Na kwamba Marekani itafanya kazi na washirika wake wa kikanda pamoja na wa kimataifa, kujadili hatua za kuchukuliwa, pamoja na namna ya kuongeza shinikizo, hasa dhidi ya wale wanaodhoofisha mchakato wa amani ama wale wanaopinga makubaliano hayo.
Rais Kiir alikuwa tayari ameonya tangu mwanzo wa mazungumzo hayo, kuwa makubaliano ya hakika yatashindikana kwa kuwa upande wa uasi umegawanyika.
Hata hivyo wapatanishi wamesema mazungumzo hayo ya amani yamepiga hatua. Mpatanishi Mkuu Seyoum Mesfin amesema ilikuwa ni siku muhimu ya mchakato wa kutafuta amani nchini Sudan Kusini. Lakini aliongeza kuwa sherehe ya kuwekwa saini, haikamiliki bila ya kuwekwa saini na upande wa serikali.
Mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo yalizuka mwaka 2013, baada ya rais Kiir kumshutumu aliyekuwa naibu wake Machar kupanga njama za kumpindua. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa asilimia sabini ya watu milioni 12 wa nchi hiyo wanahitaji misaada, huku watu milioni 2.2 wakiwa wameikimbia nchi hiyo. Na pia baadhi ya maeneo yapo katika hatari ya kukabiliwa na ukame.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/afpe
Mhariri:Josephat Charo