Kila mtu ni mlengwa vita vya Sudan Kusini
24 Aprili 2018Ripoti mpya inasema kila mtu na kila kitu ni lengo la mashambulizi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini, wakati mashambulizi dhidi ya vituo vya afya na wafanyakazi wa kutoa misaada yakiongezeka.
Karibu vituo 50 vya afya vilishambuliwa mwaka 2016 na 2017, inasema ripoti hiyo iliyotolewa jana na kundi lenye makao yake mjini New York linaloangalia hali ya watoto katika mizozo ya mapambano ya silaha. Katika karibu matukio 750 katika kipindi kama hicho misaada ya kiutu ilizuliwa na makundi kadhaa yenye silaha, ikiwa ni pamoja na majeshi ya serikali.
Majeshi ya wapinzani pamoja na yale ya serikali yameharibu kwa kudhamiria, kuchoma nyumba, kupora na kukalia majengo ya hospitali na vituo vya afya na kuwakamata, kuwateka na kuwauwa wafanyakazi wa hospitali pamoja na wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada kama mbinu ya vita, kwa mujibu wa ripoti hiyo, iliyoandikwa kwa misingi ya mahojiano ya zaidi ya watu 90 na ambayo ililenga zaidi upande wa majimbo ya Greater Upper Nile, Bahr el Ghazal na Equatoria.