1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KINSHASA : Bemba kajichimbia ubalozi wa Afrika Kusini

23 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCGR

Mgombea wa urais alieshindwa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Jean Piere Bemba ameomba hifadhi ya muda katika ubalozi wa Afrika Kusini mjini Kinshasa kufuatia mapigano ya kutwa moja kati ya walinzi wake na wanajeshi wa serikali.

Hata hivyo ubalozi huo umesema kwamba Bemba hakuomba hifadhi isipokuwa yuko kwenye ubalozi huo kwa muda kutokana na kuhisi kuwa hayuko salama baada ya kuzuka kwa mapigano karibu na makao ya Bemba kaskazini ya Gombe ambapo sauti za bunduki za rashasha,magurunedi yanayovurumishwa na maroketi na vifaru vya majeshi ya serikali zimekuwa zikisikika.

Raia wawili wameuwawa na wengine kadhaa kujeruhiwa hapo jana wakati machafuko hayo yalipozuka tena kwenye mji mkuu wa Kinshasa ambao ulikuwa shwari tokea mapigano juu ya uchaguzi wa kihistoria wa nchi hiyo kupelekea kuuwawa kwa watu 30.