1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kinshasa. DRC inatakiwa kufanya uchaguzi wa amani.

13 Septemba 2006
https://p.dw.com/p/CDCo

Mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa umoja wa Ulaya Javier Solana amesema jana Jumanne kuwa jamhuri ya kidemokrasi ya kongo ni lazima iendelee kufanya uchaguzi wa amani wakati huo huo akionya juu ya upatikanaji wa silaha nyingi nchini humo.

Solana amewaambia waandishi wa habari baada ya mazungumzo na rais Joseph Kabila na hasimu yake Jean-Pierre Bemba kuwa anaamini kuwa hali ya usalama inaimarika.

Solana alikuwa akizungumza katika makao makuu ya jeshi la umoja wa Ulaya ambalo limewekwa kulinda amani katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo sambamba na jeshi kubwa la umoja wa mataifa nchini humo, linalojulikana kama MONUC.

Hii ni ziara ya kwanza ya mkuu huyo wa sera za mambo ya kigeni wa umoja wa Ulaya kuizuru Kongo tangu kuzuka kwa mapigano baina ya vikosi vinavyomuunga mkono Kabila na vile vya Bemba hapo August 20, wakati matokeo ya mwanzo ya uchaguzi wa rais yalipotangazwa.