Kinshasa. Kabila akutana na Bemba.
14 Septemba 2006Rais wa sasa wa jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo Joseph Kabila amekutana jana na hasimu wake katika uchaguzi wa rais nchini humo Jean-Pierre Bemba kwa mara ya kwanza tangu vikosi vyao vinavyowaunga mkono kupigana mwezi uliopita.
Mkutano huo umefanyika wakati mahakama kuu ya nchi hiyo imesema kuwa tarehe ya Oktoba 29 iliyopangwa kufanyika uchaguzi wa duru ya pili ya kiti cha rais baina ya viongozi hao wawili ni kinyume na katiba.
Kwa mujibu wa katiba ya DRC , duru ya pili ya uchaguzi inapaswa kufanyika katika muda wa siku 15, mahakama hiyo imesema , licha ya kuwa katiba hiyo haifafanui kuwa ni kutokea wapi muda huo wa mwisho wa siku 15 unapaswa kuhesabiwa.
Duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais ilifanyika Julai 30.
Kabila na Bemba walizungumza kwa faragha baina yao kwa karibu saa mbili jana Jumatano jioni, kufuatia mikutano na viongozi wengine wa kisiasa na kijeshi mchana, ameeleza msemaji wa Kabila , Kudura Kasongo.