KINSHASA: Rais Kabila aongoza
10 Agosti 2006Rais Joseph Kabila anaendelea kuongoza katika matokeo ya awali ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemkrasia ya Kongo. Huku asilimia nne ya kura zikiwa zimehesabiwa, rais Kabila anaungwa mkono na asilimia 72 ya wapiga kura, akifuatiwa na Jean Piere Bemba katika nafasi ya pili ambaye ameshinda asilimia 10 ya kura kufikia sasa.
Asilimia nyegine 18 ya kura zimegawanywa miongoni mwa wagombea wengine wa kiti cha urais.
Kura zinaendelea kuhesabiwa polepole nchini Kongo huku mshindi akitarajiwa kutangazwa mwishoni mwa mwezi huu.
Wakati huo huo, msemaji wa serikali ya Kongo, Henri Mova Sakanyi, amekanusha ripoti iliyotolewa na gazeti la Uingereza kwamba Kongo iliiuzia Iran madini ya uranium.
Sakanyi amesema mgodi wa uranium wa Shinkolobwe ulifungwa rasmi mwaka wa 1960 kwa sababu ya gharama kubwa za uchimbaji wa madini hayo. Ameongeza kusema kwa sasa Kongo haiwezi kuchimba uranium na haijawahi kuiuzia Iran madini ya uranium.