1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KINSHASA : Rais Kabila kuapishwa kesho

5 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCmX

Kiongozi wa serikali ya mpito nchini Congo ataapishwa hapo kesho kuwa rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo katika kipindi cha zaidi ya miaka 40 baada ya miaka minne ya mchakato wa serikali ya muda ulitowa dosari pamoja na mambo mengine mapigano.

Sherehe hizo awali zilikuwa zimepangwa kufanyika Desemba 10 lakini msemaji wa rais Kudura Kasongo amesema zimesogezwa mbele kutokana na matokeo kutolewa na mapema kuliko ilivyopangwa. Joseph Kabila atakula kiapo katika jengo la mahkama kuu ambalo liliwaka moto wiki mbili zilizopita wakati yalipozuka mapigano na wafuasi wa mpinzani wake Jean Piere Bemba ambao walikuwa wamekusanyika kumuunga mkono wakati wa kesi yake ya kupinga matokeo ya uchaguzi yaliompa ushindi Kabila.

Wakati huo huo Tume ya Umoja wa Ulaya imependekeza kuongeza maradufu msaada wa maendeleo wa Umoja wa Ulaya kwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kusaidia ujenzi mpya wa nchi hiyo baada ya uchaguzi.

Tume hiyo imekuwa mfadhili mkubwa kwa kugharamia mchakato wa uchaguzi nchini humo tokea mwaka 2001 kwa kulipa euro milioni 165 kati ya gharama za jumla za euro milioni 400.