Kiongozi wa UEFA atafakari kubakisha ligi ya mchezo mmoja
23 Agosti 2020
Mfumo huo umetumika kwa mintarafu ya kuokoa msimu huu uliovurugika kutokana na janga la virusi vya corona hata hivyo unaweza kutumika tu katika awamu ya nusu fainali.
Katika mahojiano na shirika la habari la Associated Press siku ya Jumapili, Ceferin alisema watu ndani ya masuala ya kandanda na nje wamewasiliana nae na kusema walikuwa "wamefurahishwa mno" kutokana na mfumo wa timu nane katika fainali ambao umeachana na mfumo wa michezo miwili ya nyumbani na ugenini katika robo fainali na nusu fainali.
"Naweza kusema kuwa mfumo huu wa mchezo wa mkondo mmoja unaonekana kuleta hamasa zaidi kuliko mfumo mwingine wa michezo miwili," Ceferin aliliambia shirika la habari la AP kabla ya Paris Saint-Germain kucheza dhidi ya Bayern Munich katika fainali ya Champions League.
Ceferin alisisitiza kwamba atashauriana kwa upana kabla ya kutafuta mabadiliko ya kudumu katika mfumo.
Mfumo wa mtoano
"Ni moja kati ya mambo yenye kutia msisimko ambayo yamesababishwa na janga hili," Ceferin alisema. "Tulilazimika kufanya mfumo kama huu. Tulilazimika kucheza hivi, lakini mwishoni , tunaona ni mfumo mzuri.
"Sasa , ni hali tata sana kuweka timu nane za mwisho katika kalenda.
Lakini tuliona kuwa watu wanataka msisimko katika mchezo, ambao katika mchezo mmoja , kila timu inaweza kuishinda nyingine katika Champions League ama katika Europa League. Kwa hiyo ni kitu cha kutafakari hapo mbeleni ... Nafikiri mwezi Septemba ama Oktoba, tunalazimika kuanza kuzungumzia kwa dhati."
Ceferin hajali kwamba kuondoa idadi ya michezo ya mtoano kunaweza kuwa na athari kubwa kifedha katika UEFA.
"Hata kama una michezo michache , thamani inaweza kuwa juu iwapo itafanyiwa matangazo kwa usahihi," alisema. "Naona marafiki zangu katika kandanda na nje ya kandanda wakiwasiliana nami na kuniandikia na wote wanaonesha msisimko wa hali ya juu kwa mfumo huu. Hakuna mbinu nyingi sana uwanjani."
Makundi ya mashabiki
Kuzikusanya timu nane mjini Lisbon kukamilisha Champions League kunaonekana kuliwezekana tu kwasababu hakuna mashabiki walioruhusiwa katika viwanja viwili kama sehemu ya vizuwizi vya kusambaa kwa virusi vya corona, ikiwa na maana maafisa wa Ureno hawakulazimika kukabiliana na makundi hasimu ya mashabiki ambao wangekusanyika mitaani.
Mfumo wa timu nne za mwisho unawezekana kuchukuliwa katika mji mmoja katika muda wa wiki moja na kuleta hamasa kama ya mfumo kama wa Super Bowl nchini Marekani.
UEFA imekuwa tayari ikitafuta njia ya kubadilisha mfumo wa Champions League baada ya mwaka 2024.
Mfumo wa timu nane za mwisho tayari iliwahi kutumika kukamilisha Europa League na Champions League kwa upande wa wanawake mwezi huu.