Kiongozi wa upinzani nchini Ethiopia akamatwa
1 Desemba 2016Kiongozi wa upinzani nchini Ethiopia amekamatwa baada ya kurejea kutoka Ulaya ambako alizungumzia kuhusu hali ya hatari iliyowekwa mwezi uliopita kukandamiza maandamano dhidi ya serikali.
Merera Gudina, mwenyekiti wa chama cha Oromo Federalist Congress OFC mwenye umri wa miaka 60 alikamatwa nyumbani kwake katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa jana na anashikiliwa katika maeneo yasiyojulikana pamoja na wenzake wengine watatu, amesema Beyenne Petros, rais wa muungano wa wapinzani ambao chama cha OFC ni mwanachama.
Petros amesema kuhusiana na mwanasiasa huyo mkongwe kwamba hii ni mara ya kwanza kuwalenga viongozi wa ngazi ya juu, na kwamba Merera alikuwa akifanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria na kwa amani.
Mapema mwezi huu Gudina alihutubia bunge la Ulaya mjini Brussels, pamoja na mkimbiaji na mjumbe mwenzake kutoka jimbo la Oromo Felisa Lilesa mshindi wa medali ya fedha katika michezo ya olimpiki.