1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kitisho chagubika CAN 2010

Oumilkher Hamidou11 Januari 2010

Usalama wakati wa michuano ya fainali za kombe la dunia,baada ya mashambulio huko Cabinda

https://p.dw.com/p/LQMk
Nembo ya fainali za kombe la mataifa barani Afrika

Msiba unaogubika michuano ya kombe la mataifa barani Afrika baada ya timu ya taifa ya Togo kuhujumiwa na waasi na kuyapa kisogo mashindano hayo pamoja na minong'ono dhidi ya utaratibu wa uongozi wa kansela Angela Merkel ni miongoni mwa mada zilizotangulizwa mbele na wahariri wa magazeti ya humu nchini.

Tuanzie lakini barani Afrika, ambako mashambulio dhidi ya timu ya taifa ya Togo yamewafanya wahariri wajiulize kama fainali za kombe la dunia msimu wa kiangazi ujao nchini Afrika kusini zitakua salama.Gazeti la "TRIERISCHER VOLKSFREUND" linaandika:

"Picha za maiti na majeruhi kufuatia mashambulio ya waasi dhidi ya basi ya timu ya taifa ya Togo katika jimbo la Cabinda zinagubika michuano ya kombe la mataifa barani Afrika na ile ya fainali za kombe la dunia. Mjadala kuhusu usalama umepaamba moto. Waandalizi wanalaumiwa, hawakujiandaa vya kutosha dhidi ya mashambulio.Tangu koloni hilo la zamani la Ureno lilipojipatia uhuru mnamo mwaka 1975, jimbo hilo la Cabinda limekua kila kwa mara likigubikwa na migogoro ya mtutu wa bunduki. Waasi wanahisi eneo hilo tajiri kwa mafuta linadhibitiwa bila ya haki na Angola. Sasa kwanini michuano imepangwa kufanyika katika eneo hilo? Hata hivyo, si haki kutumbukiza kila kitu katika chungu kimoja. Hata Ulaya mashambulio yanaweza kutokea wakati wowote ule-kama ilivyoshuhudiwa wakati wa michezo ya Olympik mwaka 1972 mjini Münich. Si sawa kwa hivyo kuzusha kitisho cha mashambulio ya kigaidi, kwasababu hali kama hiyo inawatia wahka usiokua na maana waandalizi wa michuano ya kombe la dunia."

Gazeti la SÜDWEST PRESSE linaandika:

"Kimsingi michuano ya kombe la mataifa barani Afrika-CAN 2010 nchini Angola,miezi sita kabla ya fainali za kombe la dunia, ilikua idhihirishe kwa mara nyengine tena kwamba bara la Afrika sio bara la migogoro,vita na maafa. Lakini badala ya shangwe na furaha za dimba, michuano ya CAN 2010 imegeuka jinamizi hasa kwa Afrika kusini, mwenyeji wa fainali za kombe la dunia mwaka huu wa 2010. Viongozi wa kisiasa na michezo nchini Afrika kusini wanatambua fika: pindi fainali za kombe la dunia zikishindikana,mashabiki au wachezaji wakiangukia mhanga wa matumizi ya nguvu, hadhi ya bara zima la Afrika itachujuka. Wanafanya kila wawezalo ili fainali za kombe la dunia zipite salama-vikosi vya polisi vinaimarishwa na idadi yao kuzidishwa ,ushirikiano wa kimataifa kuhakikisha usalama na kampeni kubwa ya kuinua hadhi. Lakini hakuna yeyote anaeweza hii leo kudhamini kikamilifu usalama, sio barani Afrika, sio Ulaya na si kokote kwengine ulimwenguni.

Symbolbild Streitigkeiten in der Koalition
Kansela Angela Merkel na mshirika wake,waziri wa mambo ya nchi za nje Guido WesterwellePicha: DW-Montage/picture alliance/dpa

Mada yetu ya mwisho inatupeleka Berlin ambako wahariri wanajiuliza kwanini chama kidogo cha kiliberali, FDP, kinahanikiza na chama kikubwa cha CDU hakisemi mengi? Gazeti la SÄCHSISCHE ZEITUNG linaandika:

Katika mvutano wa vyama vinavyounda serikali kuu ya muungano naiwe kuhusu kupunguzwa kodi za mapato au kuhusu mwenyekiti wa jumuia ya watu wenye asili ya Kijerumani waliotimuliwa kutoka Poland, bibi Erika Steinbach, mwenyekiti wa chama cha CDU amenyamaza kimya. Zaidi ya yote, lakini, anawaweka Wajerumani katika hali ya kutojua hatua gani za kufunga mikaja watakabiliana nazo miaka inayokuja. Kwa hivyo, pale mwenyekiti wa kundi la CDU katika bunge la Sachsen, Steffen Flath, anapomtolea mwito Angela Merkel avunje miko, hapo kansela anabidi agutuke.

Mwandishi: Oumilkheir Hamidou/ Inlandspresse

Imepitiwa na: Miraji Othman