Kitisho dhidi ya Iran champonza Pompeo
22 Mei 2018Kamanda mwandamizi wa jeshi la Iran amesema umma wa Jamhuri hiyo kiislamu utampa kipigo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo kufuatia kitisho kilichotolewa na Marekani jana cha kutaka kuongeza vikwazo vikali zaidi dhidi ya nchi hiyo. Pompeo alisema serikali ya Marekani itapitisha vikwazo vikali vya kihistoria dhidi ya Iran huku akiyaonya makampuni ya Ulaya dhidi ya kuendelea kushirikiana kibiashara na Jamhuri hiyo ya Kiislamu.
Iran imekasirishwa sana na Marekani baada ya waziri wake wa mmbo ya nje Mike Pompeo kutowa kitisho dhidi ya Jamhuri hiyo ya kiislamu akisema itawekewa vikwazo vipya vya kihistoria kuhususiana na mapngo wake wa Kinyuklia ikiwa nchi hiyo hatofanya mageuzi katika mpango wake huo ikiwa ni pamoja na kuachana nao sambamba na kujiondowa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria. Leo(22.05.2018) kamanda mwandamizi wa jeshi la Iran amesema umma wa Iran utampiga ngumi ya mdomo waziri wa nje wa Marekani Mike Pompeo kutokana na kitisho chake hicho dhidi ya Iran. Rais Hassan Rouhani akizungumza jana na kundi la maprofesa wa vyuo vikuu pamoja na madaktari alisema Iran haiwezi kutishwa na Marekani wala Pompeo.
"Mtu aliyekuwa akijishughulisha wakati wote katika kituo cha ujaasusi Marekani na sasa ni waziri wa mambo ya nje anatowa matamshi ya ajabu kabisa. Anataka kuiamulia Iran na anasema Iran inapaswa kufanya hivi au vile. Hiki ni kichekesho na kituko.''
Rais huyo wa Iran alikwenda umbali zaidi wa kuyafananisha matamshi ya Pompeo na kauli zilizokuwa zikitolewa wakati wa utawala wa Gorge W Bush kabla ya kuivamia Iran mwaka 2003.
Kwa upande mwinguine waziri wa nje wa Iran Mohammad Javad Zarif pia ametoa msimamo kupitia mtandao wa Twitta na kuikosoa hotuba ya Pompeo akisema kwamba anaiona diplomasia ya Marekani kuwa fedheha ambayo imejifungia katika ndoto na sera zilizoshindwa. Uturuki nayo pia imetowa hisia zake katika suala hilo la vitisho vya Marekani kuelekea mpango huo wa Nyuklia wa Iran ambapo rais Taayip Erdogan amesema.
''Wale wanaomiliki zaidi ya vichwa vya makombora ya Nyuklia 15,000 hivi sasa wanautishia ulimwengu. Wakati wanatumia silaha hizo bila wasiwasi kwanini nchi nyingine zenye vichwa vya makombora ya nyuklia zinaonekana kwao kuwa kitisho?
Kwa nchi washirika wa Marekani barani Ulaya walisikia jinsi ambavyo Pompeo anatarajia ushirikiano wao katika mpango mpya wa Marekani lakini hakutowa ahadi yoyote kwa nchi hizo na badala yake ametishia kwamba kutakuwepo na kutoelewana kwa yeyote atakaendelea na ushirikiano wa kibisghara na Iran.Kwa maneno mengine mpango mpya wa vikwazo vya Marekani unayalazimisha makampuni ya Ulaya kuchagua ama kuendeklea na uwekezaji nchini Iran au kufanya biashara na Marekani.
Waziri wa uchumi wa Ujerumani amesema kwamba serikali itayasaidia makampuni ya Ujerumani yaliyo na biashara Iran pale itakapoweza lakini haiwezi kuyakinga kutokana na uamuzi wa Marekani.Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas atakutana Washingto Leo na Mike Pompeo kujadiliana kuhusu suala hilo la Iran. Pamoja na hayo mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini ameshasema jana kwamba hakuna mbadala wa makubaliano ya Nyuklia uliofikiwa pamoja na Iran .
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman