Kivumbi cha kutinga robo fainali Ligi ya Mabingwa
14 Machi 2016Mmoja wa miamba wa kandanda la Ulaya atabanduliwa nje, wakati Bayern Munich itapambana na Juventus siku ya Jumatano mjini Munich. Bayern, mabingwa mara tano wa Ulaya wanastahili kuhakikisha kuwa viongozi wa ligi ya Italia Juventus hawatawaharibia kampeni yao baada ya timu hizo kutoka sare ya 2-2 katika mchuano wa mkondo wa kwanza.
Katika mechi nyingine ya Jumatano, Barcelona, wanaoongoza ligi ya Uhispania, wana faida ya mabao mawili kwa sifuri dhidi ya Arsenal uwanjani Cam Nou. Barca haijashindwa mchuano hata mmoja katika mechi 37 mfululizo katika mashindano yote, na Arsenal inakabiliwa na kibarua kikali.
Kesho, Manchester City itashuka dimbani Etihad dhidi ya Dynamo Kiev ikiwa kifua mbele baada ya ushindi wake wa 3-1 katika mkondo wa kwanza. Atletico Madrid na PSV Eindhoven zitapambana katika mechi nyingine ya kesho baada ya kutoka sare ya bila bila katika mkondo wa kwanza.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP/Reuters
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman