1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Klabu za Ujerumani zatia fora UEFA

3 Oktoba 2008

Borussia Dortmund tu yapigwa kumbo nje ya Kombe la UEFA.

https://p.dw.com/p/FTSH
Borussia Dortmund yaaga UEFAPicha: AP

Baada ya duru ya kati ya wiki hii ya cha champions League , jana ilikua zamu ya kombe la Ulaya la UEFA ambamo klabu za Ujerumani hasa Wolfsburg, na Hertha Berlin zilitia fora na kuingia duru ijayo. Ni Borussia Dortmund tu ilioteleza na kupigwa kumbo nje wakati wa changamoto za mikwaju ya penalty na Udinise ya Itali jana usiku.

Klabu ya Ujerumani ya Wolfsburg na Tottenham Hotspur ya Uingereza zilikata jana tiketi zao za duru ijayo ya makundi mbali mbali kwa kombe la UEFA-kombe la shirikisho la dimba la Ulaya. Wolfsburg walibanwa sare ya bao 1:1 na Rapid Bucharest ,lakini mwishoe, ilisonga mbele kwa ushindi wa mabao 2:1 kufuatia duru ya nyumbani na ugenini.Tottenham pia ilitoka suluhu ya bao 1:1 na Krakow ya Poland na baada ya mpambano wapili inacheza duru ijayo kwa ushindi wa mabao 3-2.

Wolfsburg jana ilianza uzuri kabisa huko Rumania ilipolifumania lango la Bucharest na mapema mnamo dakika ya 15 ya mchezo.Hii iliitwika Bucharest mzigo wa kubidi kutia mabao 3 ili iweze kusonga mbele.

Tayari jumaane,klabu nyengine ya Ujerumani Hertha Berlin na ile ya Urusi CSKA Moscow zilitamba na kuwa timu za kwanza kabisa kuingia duru ijayo.Ingawa Hertha Berlin ilimudu sare tu ya 0:0 na Saint Patricks Athletic mjini Dublin katika duru ya kwanza, ilitamba Berlin na kuondoka na ushindi wa mabao 2:0.

Hamburg iliotoka sare 0:0 na Unirea Urziceni nyumbani, mwishoe ilitamba kwa mabao 2:0 huko Rumania.Schalke pia ya Ujerumani ilikwishamaliza udhia katika duru ya kwanza ya kombe hili la UEFA huko Cyprus ilijaza kikapu cha APOEL Nicosia kwa mabao 4:1 na ilitosha walipomudu sare tu nyumbani ya bao 1:1.

Borussia Dortmund ni timu pekee ya Ujerumani ilioaga mashindano ingawa kwa bahati mbaya.Kwani, Borussia ilifuta mabao 2 ya Udinese kabla haikukomewa mabao 4:3 katika changamoto za mikwaju ya penalty kufuatia kurefushwa mchezo.

Miongoni mwa matokeo mengine,Benefica Lisbon iliichapa Napoli ya Itali mabao 2-0 ili kuingia duru ijayo huku Valencia ya Spian ikishangiria ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Maritimo Funchal.

Baada ya duru hiyo ya jana ya kombe la ulaya la UEFA, klabu za Ujerumani zinajiwinda kwa Bundesliga hapo kesho:Hamburg ina miadi na Cottbus na inahitaji pointi zote 3 kubakia kileleni mwa orodha ya Ligi.Hertha Berlin iliotamba pia katika kombe la UEFA itakua na kazi ngumu kesho ikicheza na Bayer Leverkusen iliopo nafasi ya pili nyuma ya Hamburg katika ngazi ya Ligi. Werder Bremen, inafunga safari ya Stuttgart na chipukizi waliopanda msimu huu tu Hoffenheim, wanajiwinda kutoa changamoto kwa Frankfurt.

Taarifa kutoka London zasema stadi wa Ivory Coast na Chelsea, Didier Drogba atakuwa nje ya chaki ya uwanja kwa kipindi cha hadi wiki 6 kwa kuumia goti.Drogba aliumia wakati Chelsea ilipopambana na CFR Cluj ya Romania juzi jumatano.Hii yaweza kuizushia shida Chelsea katika juhudi zake za kubakia kileleni mwa premier League mwishoni mwa wiki hii-kwani masatdi wake wengine akina Deco,mghana Machael Essien,Carvalho na Joe Cole tayari hawawezi kucheza.

Kocha mbrazil Felipe Scolari , atakua na kazi ngumu jumapili hii Chelsea inapoonana na Aston villa.kuumia kwa Drogba kuna maana mfaransa Nicolas Anelka ni mshambulizi pekee wa kutumainiwa kutikisa wavu wa Villa jumapili.