Kocha wa Spurs Ange asema Kane haendi kokote kwa sasa
17 Julai 2023Katika ligi kuu ya kandanda Ujerumani – Bundesliga, mabingwa Bayern Munich wanaendelea kujikuna kichwa kuhusiana na safu yao ya ushambuliaji. Ni eneo ambalo lazima kocha Thomas Tuchel alitatue kabla ya kuanza msimu. Kwa sasa ni Dhahiri kuwa wanamuwinda mshambuliaji nyota Muingereza Harry Kane kutoka klabu ya Tottenham Hotspur. Tayari ofa mbili walizotuma miamba hao zimepigwa chini na Spurs.
Kocha mpya wa Spurs Ange Postecoglou amesema leo kuwa Kane amedhamiria kuichezea klabu hiyo hata wakati mustakabali wake ukiendelea kutiliwa mashaka. Kane anaingia katika miezi yake 12 ya mwisho ya mkataba wake wa miaka sit ana Spurs. "Kuna watu wengi wanaomjua Harry vizuri kuliko mimi, lakini hatashtushwa na chochote. Yeye yuko hapa, na wakati yuko hapa, amejitolea kabisa kwa kile tunachofanya, na hivyo ndivyo nilivyoona mambo. Kwa upande wangu, haina athari kwangu. Ikiwa watu wengine, vilabu vingine vinataka kuzungumza juu ya wachezaji wetu walio na mikataba, hilo ni suala zaidi kwao na kwetu."
Rais wa heshima wa Bayern Uli Hoeness aliongeza sauti yake katika vita vinavyoendelea vya kupata huduma za staa huyo mwenye umri wa miaka 29 kwa kuwaambia waandishi Habari mwishoni mwa wiki kuwa Kane ashafanya maamuzi kichwani ya kuhamia Bayern. Lakini Postecoglou amesema hakuna aliyezungumza naye kutoka Munich. Kane anaongoza kikosi cha Spurs kinachofanya matayarisho ya msimu mpya mijini Perth, Bangkok na Singapore
afp