1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la Afrika:Angola na Afrika kusini

22 Januari 2008

Angola inaumana jumatano hii na Afrika Kusini wakati Senegal ina miadi na Tunisia kwenye kombe la Afrika..

https://p.dw.com/p/Cw2o

Baada ya kuwaona uwanjani jana mabingwa watetezi Misri wakiumana na simba wa nyika Kamerun na mabingwa wa Afrika mashariki na kati-Sudan wakizima kwa kadiri ya uwezo wao risasi za chipolopolo-Zambia,leo ni zamu ya majirani wawili wa kusini mwa Afrika:Bafana Bafana (Afrika Kusini ) na Paa wa Angola- ya kwanza mwenyeji wa kombe lijalo la dunia 2010 na ya pili wa kombe la Afrika la mataifa mwaka huo huo. Angola inakutana na Afrika kusini huko Temale.Mpambano wapili leo ni kati ya simba wa Terange-Senegal ikiongozwa na mshambulizi wao maarufu El Hadj Diouf na ma wa afrika 2004 Tunisia.

Wakati Angola imekuwa ikiparamia ngazi ya dimba la Afrika kuja kileleni hatua kwa hatua na kuwakilisha mwaka juzi Afrika katika Kombe la dunia, Bafana Bafana-Afrika kusini chini ya kocha mbrazil Carlos Parreira, imekuwa ikiteremka ngazi hiyo tangu mbele ya mzee Madiba,ilipolitwaa kombe la Afrika la mataifa nyumbani, 1996 ilipoongozwa na nahodha wao mzungu pekee Neil Tovey.

Ni tofauti ya magoli tu ilioinyima Angola nafasi ya kushiriki katika kombe lililopita nchini Misri,miaka 2 iliopita wakati Bafana bafana walishindwa huko kuvuna hata pointi 1 au hata kutia bao.

Wakati mashabiki wa bafana Bafana mjini Soweto wangependa kuwaona watoto wao wanarekebisha dosari hiyo na kuwaigiza wenzao wa rugby waliotawaza karibuni mabingwa wa dunia,kocha mbrazil Carlos Parreira,analenga shabaha yake katika kombe la dunia 2010 nyumbani Afrika Kusini.Kwani, katika kuchagua kikosi chake kwa kombe hili la Afrika nchini Ghana,ambako ndiko alikoanzia kazi yake ya ukocha alipoifunza Black Stars na Asante kotoko,amewaweka kando wachezaji wa kongwe kama vile Ben McCarthy.Hata Macbeth Sibaya mchezaji wao wa kiungo anacheza Russia hayumo safari hii.

Kocha Parreira aliiongoza Brazil kutwaa kombe la dunia 1994 nchini Marekani ,kwahivyo atategemea leo na mechi zijazo nahodha na mlinzi wake Aaron Mokoena .

Akijua Parreira baada ya Angola,vigogo 2 vinamkabili-Senegal na Tunisia,anajua leo anahitaji ushindi na pointi 3.

Angola pia inafanya hesabu zake namna hivyo:pointi 3 zitoke kwa Bafana Bafana kwani, mbele ya simba wa Terenga au tai wa carthage,mambo huenda yakawa magumu zaidi.

Mkuki wa Angola katika lango la bafana Bafana leo utaongozwa na Mateus Goncalves .Mateues,anajua lazima atambee katika kombe hili la Afrika ili anawirishe matumaini yake ya kuichezea mabingwa wa uingereza Manchester united.Kwani, ni karibuni hivi amefunga mkataba wa miaka 3 na Manchester United.

Kinyume na majirani zao namibia waliocheza kwa mara ya pili tu juzi katika kombe la Afrika na kuchezeshwa kindumbwe-ndumbwe na Morocco walipochapwa mabao 5-1, waangola si wageni katika kombe la Afrika.hii ni mara yao ya 4.Shabaha yao itakua kuvuka duru hii ya kwanza na kucheza robo-finali kwa mara ya kwanza.Na hasa kwa vile wanae Mateus „Manucho“ akicheza bega kwa bega na mshambulizi mwengine Flavio Amado wa mabingwa mara kadhaa wa Afrika Al Ahly ya Misri.

Changamoto ya pili leo ni kati ya Tai wa Carthage-Tunisia,mabingwa wa Afrika 2004 nyumbani na simba wa Terange-Senegal.Nahodha wa Senegal El hadji diouf amerudi kuvaa jazi ya taifa kuirejesha Senegal katika heba yake ya 2002 ilipovuma kwa kishindo hadi robo-finali ya kombe la dunia.Stadi huyu wa Bolton Wanderers anatamani kuiona Senegal alao mara hii inalitwaa kombe la afrika la mataifa kama majirani zake simba wa nyika,tembo wa Ivory Coast au hata black Stars Ghana na Nigeria.

Tunisia kwa upande wake imeshatawazwa mabingwa na mramba asali-wanasema-harambi mara moja.Tegemeo lao sana leo ni Amine Chermiti.

Kocha wa Tunesia,mfaransa Roger Lemerre ameshaiongoza Ufaransa kutwaa kombe la ulaya la mataifa.Atakacho sasa ni taji la Afrika:Kwahivyo, anamtegemea sana Chermiti wa klabu ya nyumbani Etoile du Sahel kutikisa wavu wa Senegal. Senegal imezaa kizazi kipya tofauti na kile kilichousangaza ulimwengu 2002 katika kombe la dunia:

Kina jumuisha mshambulizi Mamadou Niang na Diomansy Kamara anaecheza katika premier League-Ligi ya uingereza.

Kwa mashabiki wa kusini mwa Afrika,kanda ya Cosafa inayowakilishwa na Angola,Namibia,Zambia na Bafana Bafana wangetamani timu zao kuvunja ungo katika kombe hili la Afrika na kutoa ishara ya kwanza kwamba 2010 pale Angola itakapoandaa kombe lijalo la Afrika na Afrika kusini –kombe la kwanza la dunia, ramani ya dimba la Afrika,itahamia kusini mwa afrika kutoka afrika magharibi au Afrika ya kaskazini.