Kombe la DFB : Nani zaidi Bayern na Dortmund?
27 Februari 2013Pambano hilo litakuwa ni marudio ya fainali ya kombe hilo msimu uliopita, ambapo Bayern Munich ilichezea kichapo cha mabao 5-2 dhidi ya Borussia Dortmund.
"Kwao wao ni, msimu safi kabisa , kwetu sisi lakini ni kama pambano la ugenini katika Champions League," amesema kocha wa mabingwa hao Borussia Dortmund Juergen Klopp wakati Bayern hivi sasa ikiongoza ligi ya Ujerumani kwa mwanya wa points 17, ikifuatiwa na Borussia Dortmund katika nafasi ya pili.
Kwa hiyo leo(27.02.2013) ni kati ya timu ya nafasi ya kwanza na ya pili, lakini pia ni mpambano tofauti kabisa na ligi, ambapo ni lazima leo apatikane mshindi hata kwa matuta.
Dortmund sasa inauwezo wa kuishinda Bayern
"Tunafahamu kuwa sisi ni moja kati ya timu chache katika sayari hii ambayo ina uwezo wa kuishinda Bayern. Tuna malengo yetu katika kombe hili, lakini tunahitaji kuonyesha mchezo wa hali ya juu ili kuweza kufanikisha lengo hilo leo jioni(27.02.2013).
"Huwezi kuishinda Bayern katika uwanja wao wa Allianz Arena kwa kucheza katika kiwango cha asilimia 98." amesema Klopp.
Mchezo huo katika uwanja wa Alianz Arena ni pambano la aina yake la robo fainali dhidi ya kile kinachoonekana kuwa ni timu isiyozuilika ya Bayern dhidi ya timu iliyonyakua vikombe vyote viwili muhimu katika ligi ya nyumbani Dortmund msimu uliopita.
"Hizi ni timu mbili bora kabisa nchini Ujerumani kwa sasa. Nadhani nchi nzima inashauku kubwa kuona pambano hili na sisi pia tuna shauku kama hiyo," amesema nahodha wa Bayern Philipp Lahm.
Bayern ilionja joto msimu uliopita
Baada ya kuikandamiza Bayern kwa mabao 5-2 mwezi Mei mwaka jana katika fainali ya kombe hilo, wakati mshambuliaji kutoka Poland Robert Lewandowski alipoweka wavuni mabao matatu safi kabisa , Dortmund ina uzoefu mkubwa sasa wa kuwashinda mahasimu wao wa jimbo la Bavaria katika miaka ya hivi karibuni.
Bayern haijaifunga Dortmund katika ligi ama kombe la DFB tangu Februari mwaka 2010, licha ya kuwa walifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-1 katika fainali ya "super cup" mwezi August mwaka jana dhidi ya Borussia katika wakati wa kujipasha mwili joto kujiandaa kwa kuanza msimu.
"Miaka mitatu iliyopita, bado tunachakura katika vitabu vya historia kuona lini tuliwahi kuishinda Bayern," amedokeza Klopp ambapo timu zote hizo zimo katika kinyang'anyiro cha timu 16 bora katika Champions League.
"Tumetambua kuwa Bayern wameongeza heshima yao kwetu."
Bayern imejiimarisha zaidi katika mchezo wa leo wakati kocha Jupp Heynkes aliwapumzisha wachezaji kadha nyota katika pambano la wiki iliyopita ambapo Bayern iliirarua Werder Bremen kwa mabao 6-1 katika ligi katika uwanja wa Alianz Arena.
Dortmund itakuwa na mlinzi wake Matts Hummels aliyepata maumivu katika paja, mchezaji wa kiungo Jacub , Kuba Blaszczykowski, aliyepata maumivu ya paja pamoja na mshambuliaji wake hatari Robert Lewandowski ambaye amezuiwa kucheza katika ligi kwa michezo mitatu baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu dhidi Hamburg SV.
Kabla ya pambano hilo hata hivyo kutakuwa na mpambano baina ya Stuttgart dhidi ya timu ya daraja la pili ya Bochum.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Josephat Charo