Kombe la mataifa barani Afrika na kuvunjwa Haki za Binaadam
20 Januari 2012Kesho jumamosi firimbi itapulizwa kwa michuano ya 28 ya kombe la mataifa barani Afrika.Kwa muda wa wiki tatu,timu 16 za Afrika zitapimana nguvu kuania taji la "timu bora zaidi ya dimba" barani humo.Wenyeji wa mashindano hayo,Guinea ya Ikweta na Gabon wamewekkeza fedha chungu nzima ili michuano hiyo iwe ya ufanisi.Hata hivyo mambo yakoje upande wa haki za binaadam katika nchi hizo mbili ambazo miaka ya nyuma ziligonga vichwa vya habari na sio tu kuhusiana na demokrasia?
Michezo ya Olympik mwaka 1936 nchini Ujerumani,michuano ya kombe la dunia wakati wa utawala wa kiimla wa kijeshi nchini Argentina mwaka 1978,michezo ya Olympik ya msimu wa kiangazi nchini China mwaka 2008-orodha ya nchi ni ndefu ambako michuano ya kimataifa inafanyika licha ya kwamba haki za binaadam haziheshimiwi katika nchi hizo.Mwaka 1978 fainali za kombe la dunia zilipokuwa zinafanyika Argentina,basi vituo vya mateso,vibaya zaidi katika eneo la Latin Amerika vilikuwa kilomita chache tu kutoka viwanja michuano hiyo ilikokuwa inafanyika.
Nchini China maandamano yalikandamizwa mtindo mmoja wakati wa michezo ya Ollympik.
Sasa kwa hivyo ni Gabun na Guine ya Ikweta,nchi mbili za Afrika ambazo ni mashuhuri kwa utawala wa kimabavu na kutoheshimu haki za binaadam.Katika Guine ya Ikweta kwa mfano nchi ndogo yenye wakaazi wanaokadiriwa kufikia laki saba,rais Teodoro Obiang Nguema anatawala kwa mkono wa chuma tangu mwaka 1979.Mwaka 2009 alikabidhiwa tena wadhifa wa rais baada ya ushindi unaobishwa wa uchaguzi -eti alijikingia asili mia 95 za kura.
Marise Castro,mjumbe wa Guine ya Ikweta katika shirika linalopigania haki za binaadam-Amnesty International mjini London anatoa picha mbaya kabisa ya utawala wa Obiang Ngwema na kusema:"Hali ya haki za binaadam katika Guine ya Ikweta daima ilikuwa mbaya kupita kiasi.Daima aatu wamekuwa wakikandamizwa,wanachama wa upande wa upinzani kukamatwa,mateso,watu kutiwa ndani bila ya kufikishwa mahakamani, wapinzani na wale wanaotuhumiwa kuwa wapinzani na familia zao,kesi hazifanyiki kwa haki,adhabu ya kifo,kukandamizwa uhuru wa watu kutoa maoni yao, uhuru wa watu kukusanyika,na bila ya shaka kukandamizwa uhuru wa vyombo vya habari."
Lakini hata yule ambae haandamwi na serikali,haishi kwa raha katika Guine ya Ikweta,nchi ya tatu tajiri kwa mafuta katika eneo la Afrika kusini mwa jangwa la Sahara.Rais anatumia fedha zinazopatikana kutokana na mafuta kujinunulia majumba ya anasa,magari ya anasa na vitu vyengine kama hivyo badala ya kuwekeza katika kuinua elimu,afya au kuheshimu haki za binaadam.
Hali katika nchi jirani ya Gabun ni afadhali kidogo. kwa wakaazi milioni moja na laki tano wa nchi hiyo inayoongozwa na Ali Bongo,mtoto wa kiume -tunaweza kumwita mrithi wa kiti cha enzi kilichoachwa na marehemu Omar Bongo aliyeitawala nchi hiyo kwa mkono wa chuma kwa muda wa miaka 42.Katika enzi zake ,yeyote aliyekuwa akiupinga utawala wake, Omar Bongo alikuwa akimhonga au kumuandama..
Mwandishi:Koepp,Dirke/Hamidou Oummilkheir
MhaririYusuf Saumu